Mshambuliaji wa Hamburg alikuwa mfuasi wa itikadi kali
29 Julai 2017Mwanaume huyo alietambuliwa kuwa mwenye asili ya Palestina mwenye umri wa miaka 26, aliwasili nchini Ujerumani mwaka 2015, lakini alikuwa anasubiri kurudishwa baada ya maombi yake ya hifadhi kukataliwa. Shambulizi hilo linatishia kuibua upya mjadala mkali kuhusu wakimbizi, miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu, na hivyo kuongeza shinikizo dhidi ya kansela Angela Merkel kuhusu uamuzi wake wa kuwafungulia milango waomba hifadhi zaidi ya milioni moja mwaka 2015.
"Alikuwa anafahamika kuwa mfuasi wa itikadi kali lakini siyo mpiganaji wa jihadi," alisema waziri wa mambo ya ndani wa mji huo wa bandari Andy Grote, na kubainisha kuwa "kuna viashiria vya siasa kali." Lakini waziri huyo amesisitiza kuwa japo yawezekana kukawa na lengo la itikadi kali katika shambulio hilo, mshukiwa huyo pia alikuwa na "matatizo ya kisaikolojia," na kuongeza kuwa bado haijajulikana wazi lipi kati ya hayo mawili lilimsukuma kufanya shambulio hilo.
Polisi wanaochunguzi shambulio hilo lililotokea Ijumaa jioni, wamesema mwanaume huyo aliingia dukani na kisha akachukuwa kisu chenye urefu wa karibu sentimita 20 na kumshambulia nacho mwanaume mwenye umri wa miaka 50 ambaye baadae alifariki, alisema naibu kamanda wa polisi Kathrin Hennings. Baadae aliwajeruhi watu wengine wawili katika duka hilo kabla ya kukimbia huku akiwakatakata wengine njiani, kabla ya kuzidiwa nguvu na wapita njia wenye ujasiri.
Ulinganisho na Mtunisia Anis Amri
Mashuhuda walisema mwanaume huyo alikuwa akipeperusha kisu chenye damu huku akipiga kelele za "Allahu Akbar" (Allah mkubwa zaidi) wakati akikimbia kutoka eneo hilo, lakini alifukuzwa na wapitanjia waliorusha viti kumzuwia. Ikiwa litathibitishwa kuwa shambulizi la itikadi kali, itakuwa mara ya kwanza tangu Mtunisia Anis Amri alipoendesha lori na kuwagonga watu katika soko la krismas mjini Berlin Desemba 19, na kuuwa watu 12 na kuwajeruhi wengine 48.
Ujerumani imekuwa katika hali ya tahadhari kubwa kuhusiana na kitisho cha mashambulizi ya wafuasi wa itikadi kali tangu shambulizi la Amri mjini Berlin ambalo kundi la Dola la Kiislamu lilidai kuhusika nalo. Kama ilivyo kwa mshukiwa wa Hamburg, Amri alikuwa anasubiri kurejeshwa kwao baada ya maombi yake ya hifadhi kukataliwa, lakini mchakato huo ulikwamishwa na kukosekana kwa nyaraka za utambulisho.
Tovuti ya habari ya Spiegel Online ilimtaja mshambulijai huyo kuwa Ahmad A., huku maafisa wakisema hakuwa amewasilisha rufaa dhidi ya uamuzi wa serikali kukataa maombi yake ya hifadhi. Na hata alisaidia kupatikana kwa nyaraka za kuwezesha kuondoka kwake kutoka Ujerumani. Siku ya shambulio, alikwenda hata kwa maafisa kuulizia iwapo nyaraka za utambulisho zilikuwa zimewasili.
Upekuzi haukugundua silaha kwenye makaazi yake
Mkuu wa polisi Ralf Meyer alisema mshukiwa alikuwa karibu wa kipekee katika suala hili. Polisi waliojihami kwa silaha nzito waliokagua makaazi ya waomba hifadhi mjini Hamburg alikokuwa anaishi mwanaume huyo hawakukuta silaha zozote. Katika makaazi hayo yalioko katika kiunga cha mji wa Hamburg, jirani ya Ahmad aliejitambulisha kwa jina moja tu la Mohamed, alimuelezea kama mtu mwenye akili sana.
"Alikuwa akiwasadia waomba hifadhi wengine kuhusiana na nyaraka zao," mkimbizi huyo wa Syria mwenye umri wa miaka 31 aliliambia shirika la AFP. Lakini katika wiki za karibuni, alikumbwa na mgogoro na alikuwa akisoma Quran kwa sauti kubwa chumbani kwake, alisema Mohamed.
"Na wiki tatu baada ya mfungo wa Ramadhan, alikumbwa na mgogoro mwingine. Alianza kunywa vileo na kuvuta sigara mfululizo... alikuwa mwenye huzuni kwamba mama yake alikuwa mgonjwa na kwamba maombi yake ya hifadhi yalikataliwa," alisimulia Mohamed, na kuongeza kuwa anasikitishwa kwamba kijana huyo mdogo hajafanikisha chochote maishani na sasa haelewi kwa nini alifanya vile alivyofanya.
Hofu ya kukipa hoja chama cha AfD
Wakati Ujeurmani inaelekea katika uchaguzi mkuu wa Septemba, shambulio hilo la karibuni linatarajiwa kuibua upya mjadala kuhusu rekodi ya mmiminiko wa wakimbizi. "Inakarisha sana kwamba alitenda uhalifu huo ni mtu alieomba hifadhi nchini Ujerumani na kisha akatugeuzia chuki yake," alisema meya wa mji wa Hamburg Olaf Scholz.
Beat von Storch kutoka chama cha siasa kali za kizalendo kinachopinga Uislamu cha AfD alikuwa na maneno makali zaidi, akiandika kwenye ukurasa wake wa twita kwamba "kabla bibi Merkel haja tweet tena kwamba hili halifikirikiki': hili linahusu Uislamu. Liingize hilo kichwani mwako mara moja!"
Uungwaji mkono wa chama cha AfD ulipungua kwa kiasi kikubwa katika uchunguzi wa maoni ya wananchi tangu kilele cha mgogoro wa uhamiaji, lakini chama hicho kinasalia njiani kuvuka kihunzi cha asilimia tano ya kura inayohitajika kupata uwakilishi bungeni kwa mara ya kwanza.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Lilian Mtono