MSF: Wakimbizi wa ndani Kongo wakabiliwa na ukatili
6 Agosti 2024Ripoti kutoka kundi la Epicentre, linalohudumu chini ya MSF, ambayo ilifanya uchunguzi katika kaya zinazoishi katika kambi nne magharibi mwa Goma, imesema zaidi ya mmoja kati ya wanawake 10 waliripoti kubakwa kati ya Novemba 2023 hadi Aprili 2024.
Taarifa ya MSF imesema kuwa kwa mara nyingine, waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono wanaripoti kushambuliwa na wanaume, aghalabu wenye silaha, katika misitu na viwanja ambako wanapaswa kwenda kutafuta kuni au chakula wanachohitaji kuzilisha familia zao.
Camille Niel, mratibu wa masuala ya dharura wa MSF mjini Goma amesema hali yao tete, pamoja na makazi duni ya muda wanaoishi, vinafanya kuwa katika mazingira hatari ya aina hii ya ukatili.
Kundi la waasi wa M23, ambalo lilikuwa limetulia kwa karibu muongo mmoja, lilianzisha mashambulizi katika mkoa wa Kivu Kaskazini, na kuwauwa watu kadhaa huku mamia kwa maelfu ya wengine wakiyakimbia makazi yao.