1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msalaba Mwekundu wasajili "mamia" ya wafungwa wa kivita

19 Mei 2022

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu linasema limesajili "mamia" ya wafungwa wa kivita Ukraine walioondoka kiwanda cha chuma cha Azovstal mjini Mariupol siku tatu baada ya uhamishaji wapiganaji hao kuanza.

https://p.dw.com/p/4BWlK
Ukraine-Krieg Mariupol | Abtransport von Kriegsgefangenen aus Asow-Stahlwerk
Picha: Leon Klein/AA/picture alliance

Shirika hilo la kimataifa linaloshughulikia watu walio kwenye migogoro limesema hivi leo (Mei 19) kwamba usajili wa wafungwa wa Ukraine, unaojumuishwa wapiganaji waliojeruhiwa, ulianza siku ya Jumanne kwa makubaliano kati ya Urusi na Ukraine. 

Shirika hilo limesema timu yake haikuwapeleka kwenye maeneo ambayo wanashikiliwa, ambayo hayakutajwa.

Utaratibu wa usajili, ambao unaendelea hivi leo, unajumuisha taarifa za kina kuhusu wafungwa hao kama vile majina, tarehe za kuzaliwa na jamaa zao wa karibu, kama njia ya kusaidia kuwasiliana na ndugu wa wafungwa hao wa kivita.

Tayari, Urusi ilishatangaza kwamba wafungwa hao wa kivita watahudumiwa kwa sheria zote za kimataifa kama yalivyo makubaliano kati yake na Ukraine.

Shirika la Msalaba Mwekundu limetaja baadhi ya sheria hizo zilizomo kwenye Mkataba wa Geneva kuwa ni shirika hilo kuruhusiwa kuwatembelea bila vikwazo visivyo vya lazima na kuwahoji bila kuwapo mashahidi wengine.

Ukraine yatowa msimamo mkali

Ukraine I Aufmacher I Selenskyi hält seine tägliche Ansprache an das ukrainische Volk
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine akizungumza na taifa kupitia hotuba zake za kila siku jioni.Picha: Ukraine Presidency/ZUMAPRESS/picture alliance

Wakati hayo yakijiri, mshauri mkuu wa Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema nchi yake haitakubaliana na uamuzi wowote wa kusitisha mapigano hadi pale wanajeshi wa Urusi watakapoondoka ndani ya ardhi yake.

Kauli hiyo ya Mykhailo Podolyak inaakisi msimamo wa kupindukia wa kujiamini unaochukuliwa na Ukraine wakati ikipambana na uvamizi wa Urusi.

Akiandika kupitia ukurasa wake wa Twitter, mshauri huyo, ambaye ameshirikia duru kadhaa za mazungumzo na Urusi, alisema: "Musituletee pendekezo la kusitisha mapigano - hilo haliwezekani bila ya wanajeshi wote wa Urusi kuondoka." 

Akirejelea makubaliano ya amani ya mwaka 2015 juu ya eneo la mashariki mwa Ukraine, ambayo yalisimamiwa na Ujerumani na Ufaransa na kusainiwa katika mji mkuu wa Belarus, Minsk, Podolyak ameandika kwamba: "Ukraine haina haja na 'Minsk' mpya inayofuatiwa na vita vipya ndani ya miaka michache."

Ukraine inashinda vita?

Ukraine-Krieg Mariupol | Abtransport von Kriegsgefangenen aus Asow-Stahlwerk
Msafara wa wanajeshi wa Ukraine waliojisalimisha kwa majeshi ya Urusi ukiondoka katika kiwanda cha chuma cha Azovstal.Picha: Valentin Sprinchak/Tass/IMAGO

Maafisa wengine kadhaa wa Ukraine wametowa kauli kama hiyo katika siku za hivi karibuni. Ingawa hawajaeleza kujiondowa moja kwa moja kwa Urusi kunamaanisha nini, lakini Podolyak alisema "hadi hapo Urusi itakapokuwa tayari kuyawachia huru maeneo inayoyakalia, nguvu yetu ya mapatano ni silaha, vikwazo na fedha."

Wachambuzi wanasema huenda msimamo huu wa Ukraine unatokana na tathmini ya vita inavyokwenda, ambapo mamlaka za kijeshi za Uingereza zimetaja uwezekano wa kamandi kuu ya kijeshi ya Urusi kuwa kwenye mtafaruku, wakati majenerali wa ngazi za juu wakikwepa kubeba lawama za kushindwa kwenye uvamizi mzima wa Ukraine.