Msako wakamilika bila Kony kukamatwa
9 Mei 2017Kiongozi wa kundi la waasi wa Lord Resistance Army Joseph Kony ambaye anakabiliwa na mashitaka ya kuwateka nyara maelfu ya watoto na kuwatumia kama wapiganaji au watumwa wa kingono amekuwa mbabe wa kivita mwenye sifa mbaya zaidi barani Afrika kwa miongo mitatu. Na sasa kwa vile Marekani na wengine wanahitimisha msako wao wa kimataifa dhidi yake na kundi lake la LRA, inaonekana kamwe Kony hatofikishwa mbele ya sheria.
Licha ya mamilioni ya dola kutumika katika msako dhidi yake, Joseph Kony amefaulu kukwepa mitego. Hilo ni pigo kwa wahanga wa mateso yake waliotaraji kwamba angehukumiwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague ambapo anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Wahanga walilia haki
‘‘Hamu ya haki ipo. Haki ndilo jambo ambalo watu wanataka" Amesema Judith Akello ambaye ni wakili anayeiwakilisha jamii moja ambayo wakati moja ilishambuliwa na kundi la Kony kaskazini mwa Uganda.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, kundi la Lord resistance Army limewaua zaidi ya watu 100,000. Marekani ilitoa kiasi cha dola milioni tano kwa mtu yeyote ambaye angetoa taarifa ambazo zingesaidia kufichua na kukamatwa kwa Joseph Kony. Hata hivyo hadi sasa mahali ambapo Kony yupo imesalia kuwa fumbo lililoshindwa kufumbuliwa. Waasi waliojisalimisha karibuni wa kundi lake wanasema Kony ni mgonjwa na anajificha katika msitu wa Afrika ya Kati.
Marekani yaondoa wanajeshi wake
Ikiwaondoa wanajeshi wake kwenye msako huo, Marekani ambayo ilianza kwa kuwatuma wanajeshi 100 kama washauri wa kijeshi mwaka 2011 na baadaye ikawatuma wanajeshi wa angani 150 mwaka 2014, ilisema mwezi Machi kuwa ni wapiganaji wasiozidi 100 ndio wamesalia katika kundi la LRA.
Mwezi jana, jeshi la Uganda pia lilitangaza kuwa linawaondoa wanajeshi wake 1,500 katika msako dhidi ya Kony likisema operesheni hiyo imekamilika.
Kuondolewa kwa wanajeshi kunamaanisha kuwa huenda Kony asikamatwe. Wamesema baadhi ya waangalizi. Miongoni mwa makamanda watano wa LRA ambao wameshitakiwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kibinadamu ICC, Kony pekee ndiye hajapatikana. Mmoja wa makamanda hao Dominic Ongwen aliyekamatwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati anakabiliwa na mashtaka katika ICC.
Mtafiti wa kujitegemea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati anayechunguza matukio ya LRA Kasper Agger amesema Kony amefaulu kukwepa mitego na majeshi makubwa duniani kwa miongo mitatu bila kukamatwa na kwamba waasi wa kundi lake wanaweza kujiunga na makundi mengine yaliyojihami katika maeneo ya Jamhuri ya Congo na Afrika ya Kati.
LRA lingani tisho!
Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu dhuluma za ngono katika maeneo ya machafuko inasema kundi la LRA lingali tisho kubwa katika ukanda huo. Ripoti hiyo inaongeza kuwa kundi la LRA limeendeleza mbinu zake za tangu zamani za utekaji nyara, unajisi, ndoa za lazima, kuwatunga wasichana na wanawake mimba kwa lazima kando na kuwatumia kama watumwa wa ngono katika maeneo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na pia sehemu za Jamhuri ya Congo na Sudan.
Sasha Lezhnev wa shirika la Enough Project anasema Kukamatwa kwa Kony kumeshindikana kwa sababu anajificha katika maeneo yanayodhibitiwa na Sudan ambapo vikosi vya Afrika haviruhusiwi kuendeleza operesheni. Hata hivyo Sudan imekataa madai ya Serikali ya Uganda kuwa inaunga mkono LRA.
Mchambuzi wa usalama katika eneo hilo Angelo Izama aliyeko Uganda anasema Kony na kundi lake wamekwepa ukamataji kutokana na nidhamu yao. Kauli inayorejelewa na Mathew Green ambaye ni mwandishi wa kitabu kuhusu LRA chenye anwani "Wizard of the Nile" anayesema japo Kony anaonekana kustaajabisha, aliongoza kundi la wanamgambo waliojihami vyema na waliokuwa watiifu.
Mwandishi: John Juma/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga