1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msafara wa malori ya misaada waelekea Madaya

Admin.WagnerD14 Januari 2016

Msafara wa magari zaidi ya 40 yaliyobeba misaada yameondoka mjini Damascus leo kwenda katika mji uliozingirwa wa Madaya nchini Syria, ikiwa ni msaada wa pili kwenda katika mji huo wiki hii.

https://p.dw.com/p/1HcuY
Syrien Hilfskonvoi für Madaja
Msafara wa malori kuelekea MadayaPicha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Mataifa makubwa duniani yanahimiza kile yanachoita "hatua za haraka" kupeleka misaada katika maeneo yaliyozingirwa nchini Syria kabla ya mazungumzo ya amani yanayotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.

Msemaji wa shirika la msalaba mwekundu amesema malori 44 yanaelekea mjini Madaya , ambako watu karibu 40,000 wamezingirwa na majeshi yanayounga mkono serikali kwa miezi kadhaa sasa.

Syrien Madaja Ankunft Hilfskonvoi
Watu wakisubiri msaada katika mji wa Madaya nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP/Stringer

Malori 21 mengine yanaelekea katika vijiji viwili vya Washia, vya al-Foua na Kefraya, vijiji vilivyozingirwa na waasi katika eneo la kaskazini magharibi, kiasi ya kilometa 300 kutoka Madaya.

Msaada pia umewafikia watu katika vijiji vya al-Foua na Kefraya siku ya Jumatatu.

Afisa wa Umoja wa Mataifa ameliambia shirika la habari la Reuters siku ya Jumatatu kwamba Umoja huo na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wamewaona watu walioathirika na njaa katika maeneo mawili yaliyozingirwa nchini Syria ambako misaada ilipelekwa siku ya Jumatatu.

Upelekaji wa misaada unazuiwa

Kiasi ya watu 250,000 katika mji wa mashariki nchini Syria wamezingirwa na wanamgambo wa Dola la Kiislamu ambao wanazuwia upelekaji wa misaada ya chaklula na madawa , kundi linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema.

Syrien Hilfskonvoi für Madaja
Msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa kuelekea MadayaPicha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Bei ya chakula imepanda mno katika wilaya tatu zinazomilikiwa na serikali katika mji wa mashariki ya Deir al-Zour tangu wapiganaji hao wa jihadi kulizingira na kulifunga eneo hilo mapema mwaka 2015, shirika hilo linaloangalia haki za binadamu limesema.

Ripoti za watu kufa njaa mjini Madaya , mji unaodhibitiwa na waasi ulioko milimani karibu na mpaka na Lebanon, zimesababisha malalamiko duniani. Shirika linalotoa msaada wa matibabu la madaktari wasio na mipaka limesema karibu watu 30 wamefariki katika mji huo kwa kukosa chakula tangu mapema mwezi Desemba mwaka jana.

Syrien Hilfskonvoi erreicht Madaja
Msaada uliwasili mjini MadayaPicha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Mazungumzo ya amani

Umoja wa Mataifa unasema karibu watu 400,000 kati ya watu milioni 4.5 wanaoishi katika kile inachokieleza kuwa ni maeneo " magumu kufikika" nchini Syria wanaishi katika hali ya kuzingirwa.

Staffan de Mistura / Syrien / UN
Mjumbe wa Umoja wa mataifa nchini Syria Staffan de MisturaPicha: picture-alliance/AA

Wakati huo huo mjumbe wa Umoja wa mataifa nchini Syria Staffan de Mistura ametangaza juhudi mpya za kidiploamsia katika taarifa baada ya mazungumzo mjini Geneva na mabalozi kutoka mataifa wanachama wa kudumu katika baraza la Usalama la Umoja wa mataifa : Uingereza , China, Ufaransa, Urusi na Marekani.

Wakati wa mkutano huo , mjumbe huyo amesisitiza, "umuhimu mkubwa wa watu wa Syria kuweza kupata nafasi ya wazi bila kuzuiwa kuingia katika maeneo yaliyozingirwa wakati wa kuelekea katika mazungumzo ya amani " tarehe 25 Januari mjini Geneva.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae

Mhariri: Yusuf Saumu