1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaada wa kupambana na Ebola bado wahitajika

12 Novemba 2014

Mashirika ya afya yaliyoko mstari wa mbele kupambana na ugonjwa wa Ebola, wamesema msaada wa haraka wa kupambana na ugonjwa huo bado unahitajika, licha ya kuwepo taarifa kwamba maambukizi yanapungua Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/1Dlj8
Madaktari wa kituo cha wagonjwa wa Ebola, Guinea
Madaktari wa kituo cha wagonjwa wa Ebola, GuineaPicha: picture-alliance/dpa/Kristin Palitza

Kauli hiyo wameitoa wakati ambapo Bunge la Marekani leo linatarajia kulijadili ombi la Rais Barack Obama la msaada wa dharura wa Dola bilioni 6.2 za Kimarekani kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Ebola. Mashariki hayo yanasema licha ya kuwepo taarifa za kupungua kwa visa vya Ebola, maambukizi yanazidi kuongezeka katika baadhi ya maeneo na mashirika ya misaada yamesema maelfu ya wafanyakazi wa afya wanahitaji kuwatibu wagonjwa wa Ebola katika kipindi cha miezi michache ijayo.

Andy Gleadle, wa shirika la kimataifa la madaktari wanaoyaokoa maisha ya watu na wanaotoa misaada ya kibinaadamu, anasema bado hawajafikia hatua ambayo wanaweza wakawa na ushahidi kwamba maambukizi ya Ebola yamepungua hata nchini Liberia.

Gleadle, ambaye shirika lake hilo linaendesha kituo cha matibabu nchini Liberia na lenye mpango wa kufungua vituo viwili Sierra Leone, anafafanua kuwa hata kama wataupata msaada huo wa Rais Obama sasa hivi, itachukua wiki kadhaa wa kuanza kuzitumia fedha hizo. Anasema muda zaidi unahitajika kwa ajili ya kuwapatia mafunzo wafanyakazi wapya wa afya, kujenga hospitali pamoja na kununua vifaa vya kujikinga vya madaktari na wauguzi.

Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: Win McNamee/Getty Images

Leo, Kamati ya uongozi ya Baraza la Seneti la Marekani, inatarajiwa kuwahoji maafisa wa serikali ya Rais Obama kuhusu namna nchi hiyo ilivyoupokea mripuko wa ugonjwa wa Ebola, wakati ambapo inaanza kulitathmini ombi la msaada huo.

Mchanganuo wa matumizi ya msaada huo

Dola bilioni 4.64 zitakuwa za matumizi ya haraka ya kupambana na Ebola katika eneo la Afrika Magharibi pamoja na kuiandaa Marekani katika kuongeza kasi ya maendeleo ya kujaribu chanjo ya Ebola na matibabu. Aidha, zaidi ya Dola bilioni 1.5 zitakuwa kwa ajili ya mfuko wa dharura ili kukabiliana na maendeleo ambayo hayakutarajiwa.

Ama kwa upande mwingine, serikali ya Mali leo imethibithsa mgonjwa wa pili wa Ebola nchini humo. Mgonjwa huyo ni muuguzi katika zahanati moja iliyoko kwenye mji mkuu wa Mali, Bamako. Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Ufaransa-RFI, muuguzi huyo aliambukizwa Ebola na mgonjwa kutoka Guinea, aliyekuwa akitibiwa kwenye zahanati hiyo, ambaye tayari amefariki dunia.

Waziri wa Habari wa Mali, Mahamadou Camara amesema hatua za kuzuia maambukizi ya Ebola, zinachukuliwa. Hata hivyo, waziri huyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu mgonjwa huyo. Maafisa wa Mali na wanadiplomasia wamesema mgonjwa huyo hausiani na mgonjwa wa kwanza aliyetangazwa mwezi uliopita.

Dousseyni Daou Hospital in Kayes Mali Ebola Kind
Wafanyakazi wa afya wakiwa MaliPicha: picture-alliance/AP Photo/Baba Ahmed

Mali imekuwa nchi ya sita ya Afrika Magharibi kutangaza kisa cha Ebola, baada ya msichana wa miaka miwili kutoka Guinea kufariki dunia mwezi uliopita wa Oktoba.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa idadi kamili ya watu walioambukizwa na waliokufa kwa Ebola Afrika Magharibi, ni kubwa kuliko ilivyoripotiwa. Afisa wa Umoja wa Mataifa anayeshughulika na mapambano dhidi ya Ebola, Anthony Banbury, ametoa kauli hiyo baada ya ziara aliyoifanya kwenye nchi zilizoathiriwa na Ebola za Liberia, Sierra Leone na Guinea.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,DPAE,RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman