Mripuko mpya wa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Congo
11 Oktoba 2021Wakaazi wa Beni wamepokea kwa mshangao mkubwa taarifa juu ya kuzuka upya kwa ugonjwa wa Ebola katika wilaya ya Butsili, moja wapo ya Kata za mji huu.
Kwa mujibu wa ripoti za afya kutoka Beni, kuna mgonjwa mmoja aliyeonesha dalili za Ebola katika mojawapo ya hospitali za Beni, na kwamba mgonjwa huyo alifariki dunia.
Uchunguzi wa sampuli zake za damu uliopelekwa kwenye maabara, ulionyesha kuwa mgonjwa huyo alifariki kutokana na Ebola.
Duru mbalimbali za kiafya zimesema kuwa ni watu wengine wanne waliofariki siku chache zilizopita huenda walifariki pia kutokana na Ebola.
Msaada wa haraka wa serikali
Soma pia: Congo: wahudumu wa afya wanufaika na ugonjwa wa Ebola
Akizungumza na DW kuhusu mripuko huu ambao ni wa kumi na tatu kushuhudiwa katika nchi hii, naibu mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini Edgar Mateso alisema, kuwa serikali pamoja na wafadhili wake wanapaswa kuwajibika, ili kuepuka fedheha waliyotendewa wafanyakazi katika vituo mbalimbali wanakotibiwa wagonjwa wa Ebola.
Alitumia fursa hio kutoa mwito kwa serikali kushughulikia haraka kusambaa kwa ugonjwa huo hatari.
"Ili kutokomeza haraka mripuko huu, kwetu sie watu wa mashirika ya kiutu tunadhani kwamba ni vyema kuona wizara ya afya inaleta vifaa tosha na kila kitu kinachohitajika ili kupata jibu mbashara." alisema Mateso.
Soma pia:Umoja wa Mataifa hatiani kuhusu unyanyasaji wa kingono DRC
Kampeni ya kuhamasisha raia
Ugonjwa wa Ebola ikiwa mnamo mwaka 2018 uliwaangamiza watu wengi hapa, kutokana na uzushi, duru hii wakaazi wa Beni wameonekana kuamka na tayari wameanza kuwahamasisha wenzao kuheshimu kanuni za afya.
Kuzuka upya kwa Ebola katika eneo hili kunatokea wakati nchi hii inakabiliana na virusi vya Corona pamoja na mauwaji ya kuwakata watu kwa mapanga, kumewavunja moyo wakaazi,ambao kwa sasa idadi ya vifo vinavyotokana na Covid-19 vimepungua.
Wanachokisubiri nikuona serikali inawajibika ili kukabiliana haraka na mripuko wa kumi na tatu wa ugonjwa wa Ebola katika DRC.