Mpinzani amgaragaza rais Peter Mutharika Malawi
27 Juni 2020Chama tawala cha Democratic Progressive (DPP) kimetoa wito siku ya Ijumaa kwa tume ya uchaguzi kufuta matokeo yaliojumuishwa mpaka sasa kutokana na uchaguzi huo wa pili na kutangaza kura ya tatu.
Matokeo yasiyo rasmi yaliokusanywa na kituo cha utangazaji cha serikali MBC yamempa kiongozi wa upinzani Lazarus Chakwera uongozi mkubwa wa asilimia 60, huku rais Mutharika akiwa na asilimia 39.
Matukio ya vurugu na vitisho
Katibu tawala wa chama cha DPP Francis Mphepo alisema katika taarifa kwamba kulikuwa na matukio kadhaa yenye uwezekano wa kuathiri uaminifu wa matokeo ya uchaguzi wa rais.
Chama hicho kimeorodhesha vituo vya kupigia kura ambako waangalizi wake hawakushirikishwa na kusema zaidi ya kura milioni 1.5 zilikumbwa na vurugu na vitisho.
Wapiga kura katika taifa hilo la kusini mwa Afrika walirejea katika vituo vya kupigia kura siku ya Jumanne kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi 13, baada ya mahakama ya katiba kufuta uchaguzi wa awali wa rais uliofanyika Mei 2019, kuhusiana na udanganyifu mkubwa.
Msemaji wa tume ya uchaguzi ya Malawi (MEC), Sangwani Mwafulirwa hakujibu mara moja tuhuma za chama cha DPP. "Tume inachunguza malalamiko na itatoa uamuzi karibuni," Mwafulirwa aliwaambia waandishi habari siku ya Jumamosi.
'Uchaguzi wa kuaminika kuliko wa 2019'
Matokeo kutoka wilaya 17 kati ya 28 za Malawi yalikuwa yamekusanywa na kuhakikiwa kufikia Jumamosi. MEC ina muda wa hadi Julai 3 kutangaza matokeo, ingawa tangazo linatarajiwa wiki hii.
"Tumekuwa na uchaguzi wa kuaminika sana ikilinganishwa na uchaguzi wa rais wa 2019," Mwanaharakati wa haki za binadamu wa Malawi Luke Tembo aliliambisha shirika la habari la AFP.
"Ukweli kwamba watu walijitokeza kwa wingi kupiga kura inapaswa kuchukuliwa kama ujumbe thabiti, kwamba Wamalawi kamwe hawataruhusu kura zao kuibiwa."