1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moyes: Fainali ya leo ni muhimu katika maisha yangu ya soka

7 Juni 2023

Fainali ya Ligi ya Europa Conference ya Ulaya kati ya Westham United na Fiorentina ndio kilele cha tasnia ya umeneja wa David Moyes.

https://p.dw.com/p/4SHx1
Europa Conference League - Auslosung Viertelfinale und Halbfinale
Picha: Denis Balibouse/REUTERS

Moyes amewataka wachezaji wake kumaliza ukame wa vikombe wa miaka 43 wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Premia ya Uingereza.

Klabu ya Westham haijawahi kufika fainali ya Ulaya tangu mwaka 1976 iliposhinda Kombe la Ulaya.

Fainali ya leo dhidi ya Fiorentina itakayochezwa mjini Prague itaipa klabu hiyo ya London nafasi ya kushinda taji lao kuu la kwanza tangu iliposhinda Kombe la FA mnamo mwaka 1980.

Moyes hajawahi kushinda taji kuu kama meneja.

2021 / 2022 EUFA Europa League l West Ham United vs Lyon l David Moyes
Kocha wa Westham United David Moyes akitoa maelekezo kwa wachezaji wake wakati wa pambano dhidi ya Lyon.Picha: Ashley Western/Colorsport/IMAGO

"Huu ni wakati muhimu katika tasnia yangu ya ukocha. Kuhudumu kama kocha kwa muda wote huo kunamaanisha kuwa ninafanya kitu kizuri. Hii ina maana gani kwa Westham kushiriki katika fainali ya Ulaya? Nadhani kama tungesema hivi mwanzoni mwa msimu, watu hawangeamini kama tungefika hapa."

"Ni mafanikio makubwa kufika katika fainali ya Europa Conference. Sio rahisi japo tumeonyesha ushindani na mchezo wa hali ya juu. Ni mafanikio makubwa kwa wachezaji wote na sehemu inayofuata sana ni kuona tunashinda fainali yenyewe."

David Moyes amekuwa kocha tangu mwaka 1998 na amewahi kushinda kombe katika msimu wa mwaka 1999-2000 akiwa na klabu ya daraja la tatu la Preston na ngao ya jamii mwaka 2013 wakati huo akiinoa Manchester United.

Klabu ya Westham United ilishuka dimbani mara ya mwisho mnamo Mei 28 walipofungwa na Leicester City katika siku ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu ya Premia huku wapinzani wao Fiorentina wakicheza mechi yao ya mwisho wiki iliyopita.