Moscow yaongoza kikao cha kwanza na Uturuki, Syria na Iran
10 Mei 2023Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergey Lavrov leo ameongoza mkutano wa mawaziri wenzake kutoka Uturuki, Syria na Iran kwa mazungumzo ambayo ndio ya ngazi ya juu kabisa kufanyika kati ya Ankara na Damascus tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe zaidi ya muongo mmoja uliopita. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Lavrov alielezea matumaini kuwa mkutano huo utaweka mpango wa kurejesha mahusiano kati ya Uturuki na Syria.
Amesema "Kazi yetu ni kuainisha miongozo ya jumla kwa ajili ya hatua zaidi lakini pia kuweka vigezo vya pamoja ili tusonge mbele."
Urusi kwa miaka mingi imekuwa ikijaribu kumsaidia Rais wa Syria Bashar al-Assad kujenga upya mahusiano na Uturuki na nchi nyingine ambayo yalivunjika kufuatia vita, ambavyo vimewauwa karibu watu 500,000 na kuwaacha bila makaazi wengine zaidi ya nusu ya idadi ya watu milioni 23 nchini Syria kabla ya vita.