MONROVIA : Mwanamama atarajiwa kuiongoza Liberia
12 Novemba 2005Katika mji mkuu wa Liberia Monrovia wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamefyatuwa mabomu ya kutowa machozi kuvunja maandamano ya wafuasi wa mgombea wa Urais George Weah.
Awali baadhi ya waandamanaji waliwashambulia polisi kwa mawe na kuandamana kuelekea ubalozi wa Marekani.Weah ametowa wito wa utulivu.Nyota huyo wa zamani wa kabumbu na wafuasi wake wanasema marudio ya uchaguzi wa Urais yaliofanyika nchini humo hapo Jumanne yalikuwa na udanganyifu na kutowa wito wa kusitishwa kuhesabiwa kwa kura.
Wakati asilimia 97 ya kura zikiwa zimehesabiwa mchumi wa zamani wa Benki ya Dunia Ellen Johnson-Sirleaf amejisombea asilimia 60 ya kura.Mwanamama huyo anatarajiwa kuwa kiongozi wa kwanza wa kike kuchaguliwa na wananchi barani Afrika.
Waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wamesema kwamba uchaguzi huo wa Jumanne kwa jumla ulikuwa huru na wa haki.