1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mombasa kumulikwa katika uchaguzi ujao wa Kenya

Halima Gongo24 Machi 2022

Tume ya taifa ya kutetea haki za binaadam nchini Kenya KNCHR imeyaorodhesha maeneo ya kaskazini mwa Bonde la Ufa, eneo la Nyanza na Mombasa kama baadhi ya maeneo yatakayokumbwa na dhulma za kijinsia wakati wa uchaguzi.

https://p.dw.com/p/48zcp
Unruhen in Kenia, Polizist und Demonstranten
Picha: AP

KNCHR imewaleta pamoja wadau wa kutetea haki za binaadam na vyombo vya usalama pamoja kutafuta suluhu au mbinu za kuzuia vurugu katika kaunti mbalimbali wakati huu kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao nchini Kenya.

Imesalia miezi minne pekee hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika nchini Kenya. Na tayari maandalizi yanashuhudiwa si tu kutoka kwa wanasiasa bali pia mashirika yanayoshughulika na uchaguzi nchini.

Eneo la pwani hususan mjini Mombasa ni miongoni mwa maeneo nchini Kenya ambayo yanakisiwa kukumbwa na vurugu za kijinsia wakati wa uchaguzi na tayari mikakati imeanza kupangwa mapema, kuhakikisha kuwa hali hiyo haishuhudiwi.

Kenia President Kenyatta Rede Terroranschläge 02.12.2014
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wa rais William Ruto mwaka 2014Picha: AFP/Getty Images/S. Maina

Akizungumza mjini Mombasa katika mkutano uliowaleta pamoja wadau wa kutetea haki za binaadam, Mwenyekiti wa Tume ya taifa ya kutetea haki za binaadam KNHCR, Roseline Odede amesema tayari maafisa zaidi ya 100 wamepewa mafunzo maalum kote nchini, ya kukusanya ushahidi wa vurugu zitakazoshuhudiwa kabla, baada na wakati wa uchaguzi.

Odede ametoa onyo kwa wanasiasa wachochezi, amewataka wanasiasa kufanya kampeni za amani na kutoa agizo kwa vyombo vya usalama kutoegemea mrengo wowote wa kisiasa.

Ukatili wa kijinsia umepewa kipaumbele, wadau wa tume ya KNHCR wameahidi kufanya juu chini kuhakikisha kuwa hakuna visa vya dhulma za kijinsia vinavyoripotiwa. Mkurugenzi mkuu wa tume hiyo Bernard Mogesa anaeleza kuwa wameafikiana na inspekta mkuu wa polisi kujadili njia nzuri za jinsi maafisa wa polisi watakavyofanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na raia ili kuzuia umwagikaji wa damu.Tume ya uchaguzi Kenya yapendekeza mabadiliko.

Kaunti 24 za nchini Kenya zikiwemo Kiambu, Uasin Gishu, Kisumu, Siaya, Nairobi, Wajir, Kwale, Migori, Meru, Kericho, Nyamira na Mombasa zimetajwa kuwa maeneo ambayo yana ongezeko la visa vya dhulma za kijinsia hasa wakati wa uchaguzi, vile vile ni kaunti ambazo zinaangaliwa na kufatiliwa kwa umakini hadi uchaguzi utakapokamilika.