Moja asilimia ya watu duniani ni tajiri mno
24 Januari 2018Gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung la mjini Hannover. Linazungumzia kuhusu mkusanyiko wa viongozi wa kitaifa na biashara duniani mjini Davos. Mhariri anaandika kwamba wahenga walinena kwamba hali bora ya kiuchumi katika mataifa ya magharibi yenye viwanda inaweza kuwa na matokeo mabaya hapo baadaye. Mhariri anaendelea:
Soko la hisa la Dax hapa Ujerumani limepanda na kufikia kiasi cha juu kabisa, mjini New York , Dow Jones lina paa, lakini ukilinganisha maeneo mengine ya dunia hali ni ya utegemezi kwa kila kitu. Shirika la mpango wa maendeleo la Oxfam linasema, moja asilimia ya watu wote duniani wana utajiri mkubwa ikilinganishwa na asilimia 99 ya watu duniani. Hali hii itaendelea hadi lini,? anauliza mhariri.
Baadhi ya nadharia za kale za Karl Max , aliyezaliwa miaka 200 iliyopita, zinaweza kuthibitishwa. Duniani mataifa yanafaidika sana na utajiri kwa kufanya kazi kidogo tu. Moja kati ya vitu vinavyoleta utajiri huo ni kodi ya makampuni makubwa. Trump hivi sasa anaelekea upande mwingine, anasisitiza zaidi kuhusu , "Marekani kwanza", akichukua hatua ya kupunguza kodi.
Kwa upande wa suala la kuunda serikali ya muungano nchini Ujerumani kati ya vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU na kile cha Social Democratic cha SPD, mhariri wa gazeti la Rhein-Zeitung la mjini Koblenz anaandika.
Ama wanachama wa chama cha SPD wamwangushe Schulz na kumpa mtu mwingine kiti chake , ama wamuunge mkono kwa dhati. Pamoja na hayo kiongozi huyo wa chama anatarajiwa kuwa naibu kansela katika muungano huo, akipata pia nyadhifa muhimu katika baraza la mawaziri.
Martin Schulz anaingia katika serikali bila ya uzoefu wowote wa uwaziri , nafasi ya chama cha SPD bila shaka itakuwa dhaifu katika serikali. Na kwa hiyo chama cha SPD hatimaye hakitakuwa na nafasi nzuri ukifika wakati wa uchaguzi, kwa kuwa mkuu wa chama hatakuwa na kazi nyingine tena isipokuwa kuwatuliza viongozi wenzake na wanachama ambao hawajiamini. Ni kiongozi mwenye uhakika tu na anayejua anafanya nini , anaweza kufanikiwa.
Kuhusu mjadala juu ya silaha za Ujerumani zinavyotumika na jeshi la Uturuki kupambana na Wakurdi nchini Syria , mhariri wa gazeti la Stuttgarter Nachrichten anaandika.
Si muhimu sana , iwapo ushahidi uliopo hivi sasa ni fursa pekee, kwamba mshirika wa NATO Uturuki inatumia silaha zilizotengenezwa Ujerumani katika mapambano yake na Wakurdi nchini Syria, kuweza kuilazimisha Ujerumani kutoa msimamo wake wazi. Kwa ujumla hali hii ni suala la kimaadili. Mshikamano katika NATO ni muhimu, kwa kuwa jumuiya hiyo inaihakikishia Ujerumani usalama wake. Pamoja na hayo ni muhimu kufahamu, anaandika mhariri kwamba mauzo ya silaha nchi za nje hayapaswi kuchochea mizozo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspesse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman