Mogadishu:Gedi afanya mazungumzo na wazee wa koo.
8 Agosti 2006Waziri Mkuu wa Somalia Ali Mohamed Gedi amekutana na kuzungumza na viongozi mashuhuri wa koo mbali mbali ili kutafuta maridhiano ya kuunda baraza jipya la mawaziri kufuatia kujiuzulu kwa baadhi ya mawaziri.
Mazungumzo hayo yamefanyika siku moja baada ya kuvunjwa kwa baraza la mawaziri ambalo halikukubaliana kuhusu kuwepo kwa vikosi vya kijeshi vya Ethiopia nchini humo kuilinda serikali ya mpito.
Msemaji wa serikali ya mpito ya Somalia Abdirahman Mohamed Nur Dinari amesema Waziri mkuu amefanya mazungumzo hayo na wakuu wa koo ili kujitayarisha na uundaji wa baraza jipya.
Maafisa wamesema orodha mpya ya mawaziri inatazamiwa kutolewa mnamo wiki hii, ambayo itakusanya mawaziri 31 na manaibu waziri 44.
Kiasi cha wajumbe 43 wa baraza la mawaziri walijiuzulu mwishoni mwa mwezi July wakipinga sera za uongozi wa Waziri Mkuu Gedi, hususan kitendo chake cha kuwaruhusu wanajeshi wa Ethiopia kuingia nchini mwao, kuilinda serikali yenye miezi 18 bila ya idhini ya Baraza hilo.