1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Modi amrai Zelensky kukaa mezani kumaliza vita na Urusi

23 Agosti 2024

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi anayeitembelea Ukraine amemtolea mwito kiongozi wa nchi hiyo, Volodoymyr Zelensky, kufanya mazungumzo na Urusi kwa dhamira ya kumaliza vita ndani ya ardhi ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4jreL
India Ukraine | Narendra Modi ziarani mjini Kyiv
Waziri Mkuu wa India akisalimiana na Rais Volodoymyr Zelensky wa Ukraine mjini Kyiv.Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Modi ambaye aliwasili mjini Kyiv leo asubuhi na kisha kufanya mazungumzo na Zelensky amesema anaitembelea Ukraine akiwa amebeba ujumbe wa amani na amezirai pande zote mbili kwa maana ya Ukraine na Urusi kutumia meza ya mazungumzo kutafuta suluhu.

Akizungumza kwenye kikao cha pamoja na Zelensky wakiwa wamezungukwa na maafisa wa nchi zao, Modi amesema njia ya kumaliza vita ni kupitia mashauriano ya mezani na diplomasia.

Amesema India iko tayari kuchukua jukumu la upatanishi utakaosaidia kupatikana amani. Modi ambaye ni kiongozi wa kwanza wa India kuitembelea Ukraine tangu nchi hiyo ilipojitangazia huru kutoka Dola ya Kisovieti, amesema ikiwa Kyiv na Moscow zitaona anatosha kuwa daraja la upatanishi, yuko tayari kutimiza wajibu huo kwa roho nyeupe kabisa na ya kirafiki.

Amemweleza pia Rais Zelensky kwamba India itaendelea kutoa msaada wowote wa kiutu unaohitaji wakati huu wa vita na hicho kitabakia kipaumbele cha serikali yake.

"Wakati huu wa mzozo mahitaji mengi yanaweza kujitokeza, na India imejaribu kusaidia ikiuweka mbele mtizamo wa kiutu. Ninakuhakikshia kwamba msaada wowote unaohitajika kwa msingi wa kiutu, India itakuwa nanyi na itapambana kuwaunga mkono". amesema Modi.

Zelensky asema Ukraine inataka amani chini ya misingi ya haki 

India Ukraine| Narendra Modi| Volodoymyr Zelenskyy
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alitembelea moja ya maeneo ya kumbukumbu ya vita mjini Kyiv. Alifuatana na Rais Volodoymyr Zelenskyy wa Ukraine.Picha: Indian Prime Minister’s office/AP/picture alliance

Mwito wa Modi kuhusu kutumiwa njia ya mazungumzo kumaliza vita haukutolewa majibu na Zelensky kwa sababu kiongozi huyo mwenyeji alizungumza mwanzo kabla ya kumkaribisha mgeni wake.

Lakini kwenye hotuba yake mbali ya kumshukuru Modi kwa kuizuru Ukraine, Zelensky alitetea msimamo wa nchi yake wa kutaka amani chini ya misingi ya haki.

"Suala la kumaliza vita na kupatikana amani ya haki ni kipaumbele kwa Ukraine. Sisi tulifanya mkutano wetu wa kwanza wa kusaka amani. Na ningependa kuishukuru India kwa kuhudhuria. Tunatarajia India itaunga mkono maazimio ya mkutano ule." amesema Kiongozi huyo. 

Hoja kubwa ya Ukraine imekuwa haitokubali kwenda kwenye mazungumzo chini ya matakwa ya Urusi na inapinga uwezekano wowote wa kuyaachia maeneo ya ardhi yaliyonyakuliwa na Moscow.

Urusi yasema nafasi ya kufanya mazungumzo na Ukraine imepotea 

Ukraine iliitisha mkutano wa kwanza amani nchini Uswisi mwezi Juni lakini haikuilika Urusi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov.Picha: Khalil Hamra/AP Photo/picture alliance

Mataifa ya magharibi yalihudhuria kwa wingi na India nayo ilituma mwakilishi wake. Tangu wakati huu serikali ya Zelensky imekuwa ikipambana kufanikisha mkutano wa pili ukilenga kuwaalika wawakilishi wa Urusi.

Hata hivyo mapema wiki hii waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema suala la mazungumzo halipo tena mezani baada Ukraine kufanya mashambulizi ya kuvuka mpaka kwenye mkoa wa Urusi wa Kursk.

Hadi sasa Ukraine inadai imekamata karibu vitongoji 100 kwenye ardhi ya Urusi. Moscow imejibu  kwa kufanya mashambulizi zaidi mashariki mwa Ukraine na sasa inatishia kuukamata mji muhimu wa Ukraine wa Pokrovsk na maeneo mengine ya kimkakati mashariki mwa nchi hiyo..