1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mlipuko wa bomu wajeruhi watu 17 nchini Kongo

John Kanyunyu26 Januari 2023

Wakati majeruhi wa mlipuko wa bomu katika mji wa Kasindi wilayani Beni wangali bado hospitali kuuguzwa, bomu nyingine iliripuka jana jioni mjini Beni.

https://p.dw.com/p/4MiCp
Shambulizi la tatu la bomu chini ya wiki mbili huko mashariki mwa Kongo
Shambulizi la tatu la bomu chini ya wiki mbili huko mashariki mwa KongoPicha: Zanem Nety Zaidi/Xinhua/IMAGO

Ni milango ya saa moja kasorobo ndipo mlio wa bomu uliposikika katika eneo kubwa la mji wa Beni. Bomu hilo lililitegwa kwenye jengo la mtambo wa kusagia unga wa mahindi pamoja na mihogo kwenye soko ya Macampagne, katika Kata ya Kalinda mjini Beni.

Walioshuhudia mkasa huo, mukiwemo kijana anayefanya kazi ya kusaga unga kwenye jengo hilo, wanasema, kwamba kuna mwanamume mmoja aliyeweka mfuko wake wa plastiki kwenye jengo hilo na kuondoka.

Kulingana na mashuhuda ni baada ya dakika tano ndio bomu liliripuka na kuwajeruhi watu kadhaa. 

Majeruhi walipokuwa wanapelekwa kwenye vituo vya afya kwa matibabu, maafisa wa jeshi la polisi ya Kongo pamoja na washirika wao wa polisi ya Umoja wa mataifa, waliwasili katika eneo la tukio, na kuanzisha uchunguzi, kama anavyotueleza Meleki Murara, msemaji wa polisi katika mji wa Beni.

Shambilizi la tatu la bomu

Mji wa Beni ukiwa kila mara unashambuliwa kwa mabomu ya kutengenezwa nyumbani, na shambulizi la jana likiwa linatokea siku zaidi ya kumi baada ya lile la Kasindi kwenye kanisa la madhehebu ya CEPAC, msemaji wa jeshi la polisi katika mji wa Beni anawaomba wakaazi kuwa waangalifu, huku akiwasihi kutokaribia vifurushi ambavyo hawajui vina nini ndani.

Mashambulizi ya kila uchao yanayofanywa na kundi la kigaidi kutoka Uganda ADF katika maeneo mbalimbali ya Beni, yanatokana na mkung'uto wanaoupata toka majeshi ya muungano yaani jeshi la Congo FARDC na lile la Uganda, UPDF, katika ngome zao mbalimbali, katika wilaya za Beni na Irumu.

Waasi wa Uganda wa ADF washukiwa 

Toka Novemba 2021 majeshi ya Kongo na Uganda yanaendesha operesheni za pamoja dhidi ya waasi wa ADF
Toka Novemba 2021 majeshi ya Kongo na Uganda yanaendesha operesheni za pamoja dhidi ya waasi wa ADFPicha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Msemaji wa jeshi la Congo FARDC katika sekta ya operesheni Sokola1 grand nord, captain Anthony Mualushayi aliiambia DW, kwamba ADF wakiwa hanao uwezo wa kupambana na jeshi la Kongo, wamekuwa wakilipiza kisasi kwa kuwashambulia wananchi, na kwamba, hatua madhubuti zimechukuliwa na vyombo vya dola, ili kuhakikisha kwamba mashambulizi mengine hayatokei.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wakaazi wa mji na wilaya ya Beni, kuwa wanawataarifu wanajeshi, wanapoona watu wasiojulikana katika maeneo yao, na hasa kuanzisha operesheni chunguza jirani.

Majeruhi wa shambulizi la jana, wanapatiwa matibabu, baadhi yao katika hospitali kuu ya mjini Beni na wengine katika vituo mbalimbali vya afya.

Ni watatu ndio hali yao inatajwa kuwa mahututi, kwa mjibu wa duru karibu na watabibu.

Vifo zaidi ya 3000 katika miaka mitano

Uchunguzi ukiwa unaendelea, ili kumkamata aliyelitega bomu hilo unaendelea, msemaji wa jeshi la polisi mjini Beni amesema, kuwa watatangaza matokeo ya uchunguzi huo, ili raia waweze kujua kilichotokea.

Tangu mwaka wa elfu mbili na kumi na nne, kundi la kigaidi kutoka Uganda ADF, limeshawauwa watu zaidi ya elfu tatu, katika mji na wilaya ya Beni mkoani Kivu ya Kaskazini na wilaya za Irumu na Mambasa katika mkoa jirani wa Ituri.

Na ili kuwatokomeza magaidi hao, majeshi ya Congo na Uganda, yamekuwa yakikabiliana nao katika eneo hili, yapita mwaka mmoja pamoja na miezi miwili sasa.