Mkuu wa UN awasili Kyiv kwa mazungumzo
28 Aprili 2022Guterres amepangiwa pia kulitembelea leo eneo ambalo halijafichuliwa, nje ya mji mkuu. Kama tu ilivyokuwa kwenye ziara yake ya wiki hii mjini Moscow, mojawapo ya mada zinazotarajiwa kujadiliwa ni hali katika mji wa bandari wa kusini mashariki Mariupol, ambako wanajeshi wa Ukraine na raia wamezingirwa na jeshi la Urusi.
Soma pia: Umoja wa Mataifa wahitaji dola bilioni 2.2 za msaada Ukraine
Guterres alimtembelea Rais wa Urusi Vladmir Putin na Waziri wa Mambo ya Kigeni Sergei Lavrov mjini Moscow na kisha akasafiri kwa treni kutoka Poland hadi Kyiv. Umoja wa Mataifa umesema ofisi yake ya kiutu inaunda timu yenye uzoefu kutoka kote ulimwenguni kuongoza shughuli ngumu ya kuwahamisha raia waliokwama kwenye kiwanda cha chuma mjini Mariupol kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu.
Putin atoa onyo kali
Putin alitangaza onyo lake jana akisema kuwa kama mataifa ya magharibi yataingilia mzozo wa Ukraine, yatakabiliwa na hatua za kijeshi za haraka kama umeme.
Aliwaambia wabunge kuwa Urusi ina zana za kutimiza onyo hilo, ambazo hakuna yeyote anayeweza kujigamba kumiliki, akimaanisha wazi wazi makombora ya masafa marefu ya Moscow na silaha zake za nyuklia.
Alisema hawatajisifia kuzimiliki, bali watazitumia, kama itahitajika, akiongeza kuwa wameshafanya maamuzi kuhusu hilo.
Hivyo vilikuja wakati Moscow ilidai kufanya shambulizi la kombora kusini mwa Ukraine lililolenga kuharibu shehena kubwa ya silaha zilizotolewa na nchi za Magharibi.
Wakati vita hivyo ambavyo tayari vimesababisha vifo vya maelfu ya watu vikiingia mwezi wake wa tatu, Kyiv ilikiri kuwa wanajeshi wa Urusi wameyakamata maeneo kadhaa upande wa mashariki katika jimbo la Donbas.
EU yaionya Urusi kuhusu gesi
Na katika mkwamo wake wa kiuchumi na nchi za Magharibi, Moscow ilisitisha uzambazaji wa gesi kwa Bulgaria na Poland, wanachama wawili wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO wanaoiunga mkono Ukraine katika vita hivyo. Umoja wa Ulaya umeionya Urusi kuwa hautakubali kile ilichokiita kuwa ni hujuma juu ya uungaji mkono wake kwa Ukraine, baada ya Urusi kusitisha usambazaji wa gesi kwa mataifa ya Bulgaria na Poland. Ursula von der Leyen, rais wa Halmshauri Kuu ya Ulaya, alisema Poland na Bulgaria sasa zinapokea gesi kutoka majirani zao wa Umoja wa Ulaya.
Aliliita tangazo la kampuni ya nishati ya serikali ya Urusi Gazprom kuwa ni "uchokozi mwingine kutoka Kremlin".
Alisema haishangazi kuwa Kremlin inatumia suala la mafuta kujaribu kuihujumu Ulaya…na jibu lao litakuwa la papo hapo, lenye umoja na lililoratibiwa.
Maafisa wa Umoja wa Ulaya walisema mawaziri wa nishati kutoka kote umoja huo watakutana Jumatatu kuijadili hali hiyo.
Madola makubwa ya Ulaya yameiwekea Urusi vikwazo vikali tangu uamuzi wa Putin kumvamia jirani yake, wakati yakipeleka silaha kwa wanajeshi na wapiganaji wanaoilinda Ukraine.
Soma pia: Urusi yazikatia gesi Poland, Bulgaria, EU yasema imejipanga
Lakini yamejikokota katika kulenga usafirishaji wa nje wa bidhaa za Urusi, huku wanachama wengi wa Umoja wa Ulaya – ikiwemo Ujerumani ambayo ni nchi kubwa iliyostawi kiviwanda – wakiitegemea nishati ya Urusi
Putin alijaribu kuongeza mbinyo kwa kusisitiza kuwa Urusi itakubali tu malipo ya gesi kufanywa katika sarafu ya ruble – akitumai kuwalazimu maadui wake kuongeza thamani ya sarafu yake.
Halmashauri Kuu ya Ulaya jana ilijaribu kuipa Ukraine uungaji mkono wa kiuchumi kwa kupendekeza kufutwa kwa ushuru wa kuagiza kwa bidhaa za Ukraine, lakini wazo hilo bado linahitaji kuidhinishwa kwa kura ya nchi 27 wanachama wa umoja huo.
Bruce Amani/AFP