1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa Shirika la IAEA kuizuru Iran hivi karibuni

Angela Mdungu
10 Novemba 2024

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia la IAEA Mariano Grossi amesema ataelekea Iran kufanya mazungumzo juu ya program ya nyuklia ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4mqpf
Mtambo wa nyuklia wa Bushehr, Iran
Moja mitambo ya nyuklia ya IranPicha: Iranian Presidency/ZUMA/picture alliance

Safari hiyo aliyosema itafanyika siku chache zijazo inatarajiwa, wakati kukiwa na mivutano mikali Mashariki ya Kati kutokana na vita kati ya Israel na kundi la Hamas. Itafanyika pia kukiwa na hali ya sintofahamu baada ya Donald Trump kushinda urais katika uchaguzi wa Marekani.

Soma zaidi: IAEA ina wasiwasi kuhusu vinu vya nyuklia vya Iran

Katika ziara hiyo Grossi atafanya mikutano ya ngazi ya juu na serikali ya Iran na atafanya mijadala ya kiufundi katika vipengele vyote vinavyohusiana na kauli ya Pamoja iliyokubaliwa na Iran Machi 2023.

Ziara ya Grossi inakusudiwa kutoa mwelekeao kwa ushirikiano kati ya shirika la kudhibiti nishati ya nyuklia la IAEA  na Iran kuhusu kutanua ukaguzi katika mradi wa silaha za atomiki unaozidi kukua nchini humo. Iran inaendeleza mradi huo na inaendelea kuongeza shehena ya Urani iliyorutubishwa na kufikia viwango vya silaha na kukiuka matakwa ya kimataifa, kwa mujibu wa IAEA.