NATO yaikosoa China kwa kususia mkutano wa amani kwa Ukraine
5 Juni 2024Katika mahojiano na shirika la utangazaji la Ujerumani, NDR, Stoltenberg, alisema inasikitisha kwamba China iliamua kutoshiriki mkutano huo. Uswisi imezialika takribani nchi 160 kwenye mkutano huo utakaofanyika tarehe 15 na 16 mwezi huu kujadili njia za kupata amani ya kudumu nchini Ukraine, lakini wiki iliyopita China ilitangaza kwamba haitashiriki. Akiwa mjini Beijing, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Mao Ning, amesema kuwa kuna tofauti kubwa kati ya muundo wa mkutano huo na matarajio ya China pamoja na matarajiojumla ya jumuiya ya kimataifa. Hata hivyo, Stoltenberg amesema hatua hiyo ya China sio ya kushangaza akieleza kuwa sio tu kwamba China ilishindwa kulaani uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, lakini pia Rais Xi Jinping na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, walitia saini makubaliano na kuahidiana ushirikiano usiokuwa na kikomo.