Israel yasema vita dhidi ya Hamas vitaendelea
27 Desemba 2023Mkuu huyo wa jeshi la Israel amesema mapigano dhidi ya wanamgambo wa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza wenye wakazi wengi yanafanyika katika mazingira yenye utata.
Luteni Jenerali Herzi Halevi, amesema hayo huku jeshi la Israel likizidisha mashambulizi ndani ya Ukanda wa Gaza, ambapo mpaka sasa zaidi ya watu 20,000 wameripotiwa kuuawa.
Soma Pia:Hamas, Islamic Jihad wakataa pendekezo la Misri kuachia madaraka Gaza
Wakati huo huo maafisa wakuu wa Marekani wanakutana na waziri wa maswala ya mikakati wa Israel katika Ikulu ya Marekani huku kukiwa na shinikizo la kimataifa la kusitisha mapigano. Rais wa Marekani Joe Biden amejadili na Emir wa Qatar SheikhTamim bin Hamad Al Thani juu ya kuachiliwa kwa mateka waliosalia ambao wanaoshikiliwa na kundi la Hamas wakiwemo raia wa Marekani.
Biden na bin Hamad al Thani walijadili pia juhudi zitakazowezesha kuongezeka kwa mtiririko wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza. Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za magharibi zimeliorodhesha kundi la Hamas kama kundi la kigaidi.
Soma Pia:UN yamteua Sigrid Kaag kama mratibu mpya wa misaada Gaza
Wakati hayo yakiendelea Umoja wa Mataifa umemteua naibu waziri mkuu wa zamani wa Uholanzi Sigrid Kaag kuwa mratibu wake wa maswala ya kibinadamu wa Gaza.
Kaag ni mtaalam wa maswala ya Mashariki ya Kati na jukumu lake litakuwa ni kusimamia usafirishaji wa misaada ya kwenda Gaza kama sehemu ya Azimio la Baraza la Usalama lililopitishwa siku ya Ijumaa kwa lengo la kuongeza nguvu hatua za kupelekwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Vyanzo: AFP/DPA/DW