1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa jeshi la Algeria jenerali Gaid Salah afariki dunia

Oumilkheir Hamidou
23 Desemba 2019

Kiongozi wa vikosi vya jeshi la Algeria, jenerali Ahmed Gaid Salah aliyekuwa akiiongoza nchi hiyo baada kujiuzulu rais Abdelaziz Bouteflika, amefariki dunia kwa ugonjwa wa moyo, siku nne baada ya rais mpya kuapishwa.

https://p.dw.com/p/3VH9I
Ahmed Gaid Salah
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Belghoul

Alionekana kwa mara ya mwisho hadharani decemba 19, wakati wa sherehe za kuapishwa rais mpya Abdelamjid Tebboune, aliyechaguliwa wiki moja kabla katika uchaguzi ambao mwanajeshi huyo wa miaka 79 alilazimisha uitishwe licha ya upinzani wa vuguvugu la malalamiko ya umma linalopiga nchini Algeria-Hirak.

Katika sherehe hizo rais mteule Tebboune aliwapandisha cheo rais wa muda Abdelkader Bensalah na jenerali Gaid Salah na kuwapa nishani ya "Sadr"-nishati ya wastahiki ambayo kawaida hutunukiwa viongozi wa taifa.

Baada ya kumlazimisha ajiuzulu rais Bouteflika aliyekuwa amekabwa na malalamiko makubwa ya umma dhidi ya utawala wake,  jenerali Gaid Salah akadhibiti jukwaa la kisiasa na kujitokeza kama kiongozi mwenye nguvu zaidi nchini Algeria mbele ya uongozi wa mpito wa kiraia ambao haukuwa ukisikika.

"Naibu waziri wa ulinzi, mkuu wa vikosi vya wanajeshi amefariki asubuhi" mtangazaji wa kituo cha tatu cha televisheni  ya taifa amesema , akiisoma taarifa kutoka ikulu. Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyochapishwa pia na shirika la habari la Algeria APS, jenerali Gaid Salah amefariki baada ya kupigwa na ugonjwa wa moyo akiwa nyumbani kwake, kabla ya kupelekwa katika hospitali kuu ya kijeshi ya Ain Naadja. Jenerali Gaid Salah alijiunga na jeshi  la ukombozi wa Algeria akiwa na umri wa miaka 17.

Maandamano yanaendelea nchini Algeria
Maandamano yanaendelea nchini AlgeriaPicha: picture-alliance/AP Photo

Haijulikani kifo cha jenerali Gaid Salah kitaathiri vipi shughuli za serikali mpya

Msiba wa siku tatu umetangazwa humo nchini huku jenerali Said Chengriha wa vikosi vya nchi kavu akiteuliwa kuongoza kwa muda vikosi vya jeshi la Algeria. Binafsi jenerali Chengriha aliteuliwa mwezi septemba uliopita na jenerali Gaid Salah kuongoza vikosi vya jeshi la nchi kavu.

Ni shida kuashiria kama kifo cha ghafla cha jenerali Gaid Salah kitaweza kushawishi kwa njia moja au nyengine zoezi la kukabidhiwa madaraka rais Tebboune anaesemekana alikuwa mkaribu sana wa marehemu jenerali Gaid Salah.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP