Mkutano wa shirika la afya duniani waanza Geneva Uswisi
14 Mei 2007Tatizo kubwa linatuwama juu ya ugonjwa wa kifua kikuu ambao umewaua watu wengi duniani. Nchini Ujerumani watu takriban elfu sita hufariki dunia kutokana na kifua kikuu lakini duniani kote inakadiriwa watu milioni tisa hufariki kutoka na ugonjwa huo. Kwa muda mrefu juhudi zimekuwa zikifanywa kutafuta dawa za kifua kikuu ambazo wengi hawawezi kuzifikia.
Nchini Afrika Kusini, mataifa ya Balkan na Asia Kusini, kuna aina nyingi za bakteria kama anavyosema Robert Loddenkemper, mtaalamu wa kamati kuu ya Ujerumani inayopambana na ugonjwa wa kifua kikuu.
´Tuna matokeo ya uchunguzi yanayoonyesha kuwa viluilui vinavyosababisha malaria vinatofautiana katika maeneo mbalimbali, katika maumbile na ukali wa hatari. Na pengine hiyo ndiyo funguo ya ufanisi katika siku za usoni. Pengine ni muhimu kutengeneza chanjo tofauti kukidhi mahitaji ya kila eneo.´
Utengenezaji wa chanjo mpya dhidi ya kifua kikuu una gharama kubwa mno. Shirika la afya duniani limebaini kuwa chanjo hiyo haitaweza kupatikana kabla mwaka wa 2012. Dawa inayotumika kwa sasa imepitwa na wakati na hapo ndipo kulipo na tatizo. Kwa mujibu wa shirika la ´Madaktari wasio na Mipaka´ kwa muda mrefu hakujakuwa na ari ya kutaka kutengeneza dawa mpya ya kifua kikuu kwa sababu ugonjwa huo haupatikani sana Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi.
Mwanachama wa shirika la madaktari wasio na mipaka, Schön-Angerer, amesema hiyo ndiyo sababu kampuni za kutengeneza dawa hazijajitolea kuwekeza kwa kuwa hamna faida inayotarajiwa. Shirika la afya duniani kwa hivyo linakabiliwa na changamoto kubwa.
´Shirika la afya duniani, WHO, haliwezi tu kufuata njia ya utulivu ya kisiasa bali linawajibika kufuatilia mzozo wa sasa kuhusu siasa za haki miliki. Linatakiwa pia kutumia nafasi ya kihistoria kuweza kufikia makubaliano kuhusu utafiti na maendeleo ili kuvumbua aina mpya ya dawa na njia za kutambua magonjwa hususan katika maeneo zinakotakikana kwa dharura, kwa mfano ugonjwa wa kifua kikuu.´
Hali ni hiyo hiyo katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa ukimwi. Kuna dawa nyingi nzuri za kupunguza makali ya ugonjwa huo ambazo ni za gharama kubwa kwa mataifa ya Afrika au barani Asia. Ndio maana wagonjwa katika maeneo hayo hawanufaiki kutokana na uvumbuzi mpya wa dawa. Kampuni za dawa zinataka kutengeza dawa zitakazoweza kuuzwa katika masoko ya nchi za mabara hayo.
Ili kuweza kupiga hatua angalau moja mbele, wajumbe wa mkutano wa mjini Geneva Uswisi wana siku tisa pekee kujadiliana kujaribu kulifikia lengo hilo.