Mkutano wa Munich wamalizika kwa miito ya kuisaidia Ukraine
19 Februari 2023Katika siku ya mwisho mkutano huo ambao kila mwaka mwaka uwaleta pamoja maafisa wa ngazi ya juu duniani kujadili masuala ya usalama, viongozi kadhaa wa Ulaya walijikita katika kujadili hatma ya usalama wa bara hilo siku za usoni.
Suala jingine muhimu ni miito iliyotolewa na baadhi ya mataifa ya Ulaya ya kutaka Ukraine isaidiwe kupata silaha zaidi kupambana na Urusi.
Wakati vita kati ya Urusi na Ukraine vinaelekea kutimiza mwaka mmoja mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell amesema anaunga mkono pendekezo la Umoja wa Ulaya kununua silaha zaidi kwa niaba ya nchi wanachama kuisaidia Ukraine.
Matamshi hayo ameyatoa baada ya waziri mkuu wa taifa dogo la Baltiki la Estonia, Kaja Kallas kutoa shauri hilo alipozungumza kwenye mkutano wa usalama mjini Munich.
``Ninakubaliana kikamilifu na pendekezo la Waziri mkuu wa Estonia na tunalifanyia kazi na litafanikiwa `` amekaririwa akisema mwanadiplomasia huyo mkuu wa Umoja wa Ulaya.
Pendekezo hilo laungwa mkono na viongozi wengine wa EU
Wazo hilo la kukusanya nguvu za mataifa wanachama badala ya kila taifa kutuma msaada binafsi kwa Ukraine linaungwa mkono pia na rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema litasaidia pakubwa kuipatia Ukraine silaha za kutoka.
Uingereza imesema yenyewe iko tayari kuratibu mpango wa mataifa ya Ulaya yenye nia ya kuipatia ndege za kivita Ukraine. Hilo limesemwa na Waziri mkuu Rishi Sunak mjini Munich ambaye ametoa pia wito kwa washirika wa Ukraine kutoitupa mkono nchi hiyo.
Poland kwa upande wake imesema iko tayari kuipatia Ukraine ndege za kivita chapa MiG lakini hadi pale muungano wa msaada wa aina hiyo utakapoundwa chini ya uongozi wa Marekani. Hayo ni kulingana na Waziri mkuu wa Poland.
Marekani yasema Urusi imetenda uhalifu wa kivita Ukraine
Katika hatua nyingine Urusi imekasirishwa na matamshi ya Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Haris, aliyesema Washington imejiridhisha kuwa Urusi imetenda uhalifu dhidi ya ubinadamu katika vita nchini Ukraine.
Kamala amesema hayo akiwa mjini Munich alikokuwa anahudhuria mkutano wa masuala ya usalama uliomalizika siku ya Jumapili.
Kwa mujibu wa serikali ya Marekani, mashirika yanayofadhiliwa na shirika la misaada la nchi hiyo USAID, yameorodhosha zaidi ya matukio 30,000 ya uhalifu wa kivita, tangu kuanza kwa uvamizi huo wa Urusi Februari 24 mwaka jana.
Tume ya uchunguzi inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa pia inasema imebaini uhalifu wa kivita lakini haijahitimisha iwapo unafikia uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Urusi imejibu msimamo huo wa Marekani kupitia balozi wa Urusi mjini Washington Anatoly Antonov ambayo amekanusha vikali madai hayo akisema Washington inajaribu kuchochea mzozo na chuki dhidi ya Urusi kupitia madai hayo.