Mkutano wa Majadiliano wa Libya wakosa makubaliano
16 Novemba 2020Kaimu Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Libya, Stephanie Williams, amewaambia waandishi wa habari kwamba wameamua kuendelea na mkutano mwengine ndani ya wiki moja kuhusu jinsi ya kuupata uongozi huo.
Mkutano huo wa wiki moja, ambao ulikuwa hatua ya hivi karibuni kabisa kusaka suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Libya, uliwahusisha wajumbe 75 waliochaguliwa na Umoja wa Mataifa kuwakilisha makundi muhimu ya Libya.
Wajumbe hao walipewa jukumu la kubuni mpango wa kuipeleka Libya kwenye uchaguzi, kuamua juu ya mamlaka utakayokuwa nayo uongozi wa serikali ya mpito na kuwataja wajumbe wa serikali hiyo.
Awali, mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alikuwa amesema kwamba washiriki wa mazungumzo hayo yaliyokuwa yakifanyika kwa njia ya mtandao kutokea nchini Tunisia "walikubaliana kwamba uchaguzi mkuu utafanyika tarehe 24 Disemba mwakani, ikisadifiana na maadhimisho ya miaka 70 ya uhuru wa Libya."
Mazungumzo ya sasa yanafanyika wakati Libya ikiwa kwenye shinikizo kubwa la kimataifa kuumalia mzozo ambao unakaribia miaka kumi sasa, tangu kupinduliwa na kuuawa kiongozi wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika, Muammar Gaddafi.
Kazi ngumu
Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wamekosowa njia iliyotumika kuwapata wajumbe hao, wakitilia mashaka utiifu wao kwenye nchi ambayo tayari ina serikali mbili zinazopingana, makundi kadhaa yenye silaha na mataifa ya kigeni yanayowania ushawishi.
Juhudi za kidiplomasia za hapo awali kuumaliza mzozo huo zimekuwa zikivunjika kila mara.
Mwezi uliopita, pande hasimu zilikubaliana kusitisha mapigano kwenye makubaliano yaliyosimamiwa pia na Umoja wa Mataifa mjini Geneva.
Utawala wa taifa hilo tajiri kwa mafuta hivi sasa umegawika baina ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa yenye makao yake kwenye mji mkuu, Tripoli, na ile inayoongozwa na waasi mashariki mwa nchi hiyo.
Pande hizo mbili zinaungwa mkono na makundi mbalimbali yenye silaha, na pia mataifa jirani na ya kigeni.
Vikosi vya mashariki vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Hiftar vilianzisha mashambulizi ya kujaribu kuutwaa mji mkuu Tripoli mwezi Agosti 2019.
Lakini operesheni hiyo ilishindwa mwezi Juni, baada ya wanamgambo wanaoiunga mkono serikali mjini Tripoli kupata msaada mkubwa kutoka Uturuki na kuwarejesha nyuma wapiganaji wa Hiftar.