1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa msitu wa Amazon wafanyika Brazil

8 Agosti 2023

Mji wa Belem nchini Brazil ni mwenyeji wa mkutano wa kilele wa msitu wa Amazon ambapo watunga sera na maafisa wengine wanakutana kujadili jinsi ya kukabiliana na changamoto kubwa za kulinda chanzo muhimu cha mazingira.

https://p.dw.com/p/4UtQi
Msitu wa Amazon
Picha ya juu ya msitu wa Amazon Picha: ALAN CHAVES/AFP via Getty Images

Msitu wa mvua wa Amazon una ukubwa wa mara mbili wa nchi ya India na unapatikana katika nchi nane. Ni msitu muhimu kwa kunyonya gesi chafu ya kaboni, una asilimia 20 ya hifadhi za maji safi duniani na una takriban spishi 16,000 za miti.

Ila serikali zimeuchukulia msitu huu kama eneo la kukoloniwa na kutumika vibaya pasi na kuzingatia haki za watu asili wanaoishi katika msitu huu. Lakini kipi ni kitisho kikubwa cha kimazingira kwa msitu wa Amazon?

Kilicho juu kwenye orodha ya vitisho hivyo ni ukataji wa miti. Msitu wa Amazon umepoteza zaidi ya ekari milioni 211 au asilimia 13 ya eneo lake la asili. Sehemu kubwa ya uharibifu huo umefanyika katika nusu karne iliyopita huku Brazil, ambayo ni mwenyeji wa thuluthi mbili ya msitu huo, ikiwa sehemu iliyoshuhudia uharibifu mkubwa.

Soma hapa juhudi za kulinda msitu wa Amazon: Ujerumani yaahidi kusaidia ulinzi wa msitu wa Amazon

Maafisa wa kuzima moto katika msitu wa Amazon
Msitu wa Amazon uliwahi kukumbwa na moto mkubwa wa nyikaPicha: Bruno Kelly

Hakuna sehemu iliyo na uharibifu mkubwa zaidi kuliko jimbo la Para ambalo mji wake mkuu ni Belem. Asilimia 41 ya ukataji miti katika msitu wa Amazon Brazil umefanyika katika jimbo la Para, ambako sehemu kubwa ya ardhi imebatilishwa na kufanywa eneo la kufuga ng'ombe milioni 27. Kulingana na mtandao mmoja wa makundi ya kimazingira, hili ndilo eneo linaloongoza kwa utoaji wa gesi chafu katika majimbo ya Brazil.

Kitisho chengine cha mazingira ni mabwawa makubwa ya kufua umeme hasa nchini Brazil, uchimbaji madini na mafuta huku mambo hayo yakiwa na athari kwa maji na kuyatatiza maisha ya watu wa asili.

Kutoekeza kikamilifu katika miundo mbinu ni jambo linalomaanisha kwamba sehemu kubwa ya maji machafu kutoka majumba yaliyoko katika msitu huo wa mvua, yanaingia moja kwa moja kwenye njia za maji. Msitu wa Amazon katika miaka ya hivi karibuni pia umeshuhudia mafuriko na ukame.Amazon, makampuni makubwa yaahidi kuajiri maelfu ya wakimbizi

Mambo mengine ambayo ni kitisho kwa msitu huu ni ujenzi wa barabara na uhalifu. Awali serikali katika maeneo hayo zilikuwa zikitengeza barabara katika msitu huo kwa kukata miti tu ila mvua zimekuwa ziharibu barabara hizo. Kutokana na hilo, ikachukuliwa hatua ya kuzitia lami ili iwe rahisi pia kwa usafirishaji wa bidhaa za kilimo.

Hili ni jambo zuri ila liliwasaidia wavunjaji sheria kufika maeneo ya ndani kabisa ya msitu huu na kukata miti kwa ajili ya ufugaji miongoni mwa mambo mengine.

Soma pia: Uharibifu wa mazingira huenda ukaongezeka Brazil

Chengine kilichochangia kwa mashirika ya kihalifu kukita mizizi msituni humo ni ufisadi na kulemaa katika masuala ya utekelezaji wa sheria. Maeneo machache ya mpakani yana ulinzi mkali wa polisi na kumekuwa ushirikiano mdogo wa kimataifa, wakati ambapo magenge ya wahalifu yanashindana kwa njia za ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Lakini msitu wa Amazon ni muhimu kwa kiasi gani katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi? Athari za mabadiliko ya tabia nchi hua mbaya zaidi pale mimea ya kuinyonya gesi chafu ya kaboni inapopotea na msitu wa Amazon una umuhimu mkubwa katika kunyonya gesi hii ya kaboni.

Mwanakemia Luciana Gatti, aliyekuwa mwandishi mwenza katika jarida la Asili, lililobaini kuwa eneo la mashariki la msitu wa Amazon lililoshuhudia ukataji mkubwa wa miti, kwa sasa hivi halifyonzi tena gesi ya kaboni na badala yake ni chanzo cha gesi hiyo. Gatti anasema nusu ya eneo la Amazon mashariki lililokatwa miti linastahili kupandwa miti hiyo, ili msitu huo wa mvua uendelee kusalia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ila maendeleo yanaweza kufanyika katika msitu huu wa Amazon bila uharibifu wa mazingira? Marcelo Salazar, mkongwe wa kazi za ushauri na mazingira anasema, msitu huu ni mkubwa mno na unakanganya kiasi cha kwamba hakuna suluhu moja la maendeleo katika maeneo tofauti.

Salazar anasema kwanza serikali zinastahili kutoa haki za kiafya, kielimu na ulinzi wa ardhi ili uchumi wa msitu huo uweze kufanya kazi kikamilifu. Chengine anachopendekeza Salazar ni, kueleimishwa kwa watu wa asili kwenye msitu huo kuhusiana na jinsi ya kuwasilisha changamoto za msitu huo kwa ajili ya kuwasaidia walioko nje kuuelewa na pia kuwavutia wawekezaji.

Chanzo: APE