Mkutano wa kilele wa G20 waanza Hamburg
7 Julai 2017Viongozi wote wa nchi wanachama wa kundi la G20 wamekwishawasili mjini Hamburg, wa mwisho kutua asubuhi ya leo akiwa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Muda mfupi uliopita mwenyeji wa mkutano huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewakaribisha viongozi wenzake, huku maafisa wakifanya juhudi kubwa nyuma ya pazia, kutafuta muafaka kuhusu maazimio ya mkutano.
Lakini licha ya kauli mbiu ya mkutano huo inayotaka 'Dunia iliyounganishwa', kuna pengo kubwa kimtazamo baina ya viongozi muhimu katika kundi hilo, kuhusu masuala muhimu kama biashara na mabadiliko ya tabia nchi. Hakuna tofauti kubwa kati ya viongozi hao kuhusu suala jingine muhimu, ambalo ni mkakati wa kupambana na ugaidi.
Trump atarajiwa kuwa kikwazo
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anataka kupigia debe biashara huria, lakini anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump, kutokana na sera yake ya 'Marekani kwanza'. Hata hivyo, akizungumza kabla ya kuanza mkutano huo, Kansela Merkel amesema anayo matumaini ya kupatikana muafaka, na kusema miongoni mwa mengine, hilo litakuwa jukumu kama kiongozi wa nchi mwenyeji.
'Ukweli kwamba nchi yetu ni mwenyekiti wa mkutano, unamaanisha kuwa nitasimamia maslahi ya Ujerumani na ya Ulaya katika mkutano wa kilele wa G20. Kwa upande mwingine lakini, kama mwenyeji nitatafuta muafaka ili kupata majibu kuhusu namna utandawazi unavyoweza kuendeshwa.'' Amesema Kansela Merkel.
Wachambuzi wanasema tayari Bi Merkel amekwishapunguza matarajio kuhusu yatakayokubaliwa katika mkutano huu, kutokana na changamoto zilizoshuhudiwa katika mkutano wa kilele wa nchi saba zinazoongoza kiuchumi duniani, uliofanyika Sicily, Italia mwezi Mei mwaka huu.
Hatimaye Trump na Putin wakutana
Kama ilivyotokea katika mkutano huo, Rais Donald Trump wa Marekani anatarajiwa kuchukuwa msimamo unaokinzana na viongozi wengine, hususan kuhusu biashara na mabadiliko ya tabianchi. Muswada wa azimio la mkutano huo, ambao nakala yake imepatikana kwa shirika la habari la Ujerumani, DPA, inaonyesha Trump akitengwa na viongozi wengine waliokusanyika mjini Hamburg.
Pembezoni mwa mkutano huu, itafanyika mingine kadhaa baina ya viongozi wanaohudhuria, huku ule kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na wa Urusi Vladimir Putin, ukihofiwa kuweka kiwingu juu ya mkutano rasmi wa G20. Itakuwa mara ya kwanza kwa viongozi hao kukutana ana kwa ana, tangu Trump alipochaguliwa kuwa rais wa Marekani.
Mkutano huo tangu jana unagubikwa na maandamano makubwa ya mamia ya maelfu ya watu wanaopinga utandawazi, ambao wamechoma moto magari na kuweka vizuizi katika barabara za Hamburg. Helikopta za polisi zinazunguka katika anga la mji huo, kuhakikisha usalama.
Mbali na mada kuu za mkutano huo, viongozi wa G20 watajadili pia mzozo wa Syria, na kitisho cha mpano wa makombora na silaha za atomiki vya Korea Kaskazini.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae,rtre,dw
Mhariri: Josephat Charo