1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Geneva juu ya wakimbizi wa Irak

17 Aprili 2007

Leo na kesho wajumbe kiasi cha 450 kutoka nchi 60 mbali mbali wanazungumzia hatima ya wakimbizi kiasi cha milioni 4 wa kiiraki-nusu wakiwa nje ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/CHG9

Leo unafanyika mkutano wa siku mbili huko Geneva,kwenye kituo cha Umoja wa mataifa.Mada kuu ni hatima ya wakimbizi wa Irak.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi (UNHCR) limewaalika wajumbe 450 kutoka nchi 60 mbali mbali pamoja na mashirika mengine kadhaa ya misaada.

Idadi ya wakimbizi wa Irak imefikia sasa milioni 4.Nusu yao wameweza kukimbilia nchi za n’gambo katika nchi jirani na Irak -Jordan na Syria.

Nusu nyengine wakimbizi kiasi cha milioni 2 wamekwama nchini Irak.Baadhi yao wanazurura bila kujua wakimbizia wapi roho zao.Ni watu wasio na pa kukaa au kazi kwa muujibu yasemavyo mashirika ya misaada.

Bibi Beatrice Megevand anaelihudumia shirika la Msalaba mwekundu kwa wakimbizi wa kiirak anasema:

“Wakimbizi hawa wana upungufu wa kila kitu.Kuna upungufu wa madawa na maji safi.Hili ndilo tatizo kuu hasa-kupata maji safi kwa watu hawa. Mara nyingi hupatikana maji ,lakini ni maji machafu hayafai kunywa.Hasa mtu asisahau kuwa, zaidi ya nusu ya wakimbizi waliotimuliwa nchini Irak ni watoto wadogo-watoto ambao hata hawakufikia umri wa miaka 12.”

Kiasi cha dala milioni 60 kinahitajika mwaka huu pekee kwa makisio ya shirika la UM la wakimbizi UNHCR kuwahudumia wakimbizi wa Irak.Kwa muda mrefu ujao zitahitajika hadi dala bilioni.

Lakini, fedha ni tatizo moja tu anaongeza Bibi Beatrice Megevand wa shirika la msalaba mwekundu:Tatizo jengine ni upungufu wa watumishi wa kuwahudumia wakimbizi hao katika sehemu mbali mbali za Irak.

“Hospitali nyingi na vituo vya matibabu zinajikuta kati kati ya maeneo ya mapigano.Watumishi wake wengi kutokana na hali ya usalama wameihama Irak.Kwahivyo, kuna kosoro ya takriban kila kitu-wauuguzi,madaktari na hata madawa.”

Hata waziri wa nje wa Irak anatazamiwa leo na kesho kuhudhuria kikao hiki mjini Geneva.Mojawapo ya mada kuu kabisa ambazo wajumbe kutoka nchi 60 mbali mbali na mashirika yasio ya kiserikali watazizingatia, ni ukosefu wa mamlaka ya kutawala barabara kwa serikali ya sasa ya Irak.

Dennis McNamara,mjumbe wa UM anaewashughulikia wakimbizi anasema:

“Tatizo kuu kwa mashirika ya misaada ni usalama. Hatuna kabisa usalama katika sehemu nyingi za Irak.Na hali hii katika kipindi kifupi kijacho haitabadilika .

Ndio maana pande zinazogombana nchini Irak, zina jukumu maalumu.Nalo ni kuwashughulikia raia na kuhakikishia kuwa mashirika ya misaada yaweza kufanya kazi zao kwa usalama.”

Kwa hali ilivyo sasa, bila ya watumishi wa kiiraki hakuna kinachoenda.Kwani hali ni hatari sana na hii amethibitisha Rafiq Tschannen,kiongozi wa miradi mbali mbali ya shirika la kimataifa la wahamiaji.

Tschannen na wajumbe wengine wengi katika kikao cha leo mjini Geneva, wanatarajia kwahivyo, pataibuka mkakati utakaofafanua vipi shughuli za kiutu ziendeshwe nchini Irak katika halio ya sasa.