Mkutano wa Geneva dhidi ya ubaguzi
21 Aprili 2009Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wamemulika zaidi mkutano wa Umoja wa mataifa dhidi ya ubaguzi mjini Geneva.Hata hivyo maridhiano kuhusu kodi za mapato yaliyofikiwa na washirila wa serikali kuu ya muungano na maonyesho ya kimataifa ya mjini Hanover nayo pia yamezingatiwa.Tuanze lakini na mkutano wa Umoja wa mataifa dhidi ya ubaguzi,uliofunguliwa jana mjini Gevena.Gazeti la "BADISCHE ZEITUNG la mjini Freiburg linaandika:
Mataifa mfano wa Ujerumani yalitambua mapema,kilichokusudiwa na Iran katika mkutano huo na ndio maana yameamua kutoshiriki.Hayajakosea.Yasingeweza kukubali Israel ikashifiwe.Kwasababu hata kama lawama dhidi ya siasa ya Israel kuelekea wapalastina si za bure,hata hivyo ,kinyume na anavyohoji Ahmadinedjad,ubaguzi sio chanzo cha mzozo huo.Chanzo ni mvutano wa jamii mbili kwa ardhi ambayo kila upande unaidai.Anaetaka kuufumbua mzozo huo anabidi aanzie hapo.Lakini hicho sicho anachokitaka Ahmadinedjad.Yeye anatafuta mabishano tuu.Inasikitisha kuona analitumia vibaya jukwaa la umoja wa mataifa ambalo lengo lake ni la maana,nalo ni kuupiga vita ubaguzi."
Gazeti la "Saabrücker Zeitung linakosoa ile hali kwamba kuna mataifa yanayosusua mkutano huo wa kimataifa dhidi ya ubaguzi.Gazeti linaendelea kuandika:
Mkutano huo wa Uswisi hautokani na juhudi za waimla.Waandalizi wa mkutano huo ni Umoja wa mataifa.Na hii ni mara ya kwanza kwa Ujerumani kususia mkutano mkubnwa kama huo wa Umoja wa mataifa.Kwa namna hiyo Ujerumani inaharibu pia sifa ya Umoja wa mataifa.Ingekua bora zaidi pindi Ujerumani ingetoka nje ya ukumbi kulalamika dhidi ya matamshi ya chuki ya Ahmadinedjad.Anaetaka kuepukana na ugonvi mapema,asishangae anapojikuta akikosolewa kwamba amewaachia jukwaa la Umoja wa mataifa wale wanaotoa matamshi ya chuki dhidi ya Israel.Ili kuweza kushawishi mambo,mtu asiiachie fursa kupita,lazma achangie na hasa katika jukwaa la Umoja wa mataifa:
Mada ya pili magazetini hii leo inahusu maridhiano katika ugonvi kuhusu mswaada wa sheria dhidi ya wanaohamishia mali ng'ambo ili kuepuka kulipa kodi za mapato.Gazeti la General Anzeiger linaandika:
Serikali kuu ya muungano inaonyesha imekubaliana hatimae kuhusu hatua za pamoja za kupambana na wanaohamishia fedha nchi za nje ili kukwepa kulipa kodi.Hata hivyo makubaliano hayo sio sababu ya kudanganyika na kufikiri kwamba hakutokua tena na msimamo wa pamoja linapohgusuka suala la sera ya pamoja ya kodi na fedha katika serikali kuu ya muungano.
Mwandishi:O.Hamidou
Mhariri:M.Abdul-Rahman