Mkutano wa G7 kujadili mzozo wa Mashariki ya Kati
17 Aprili 2024Waziri wa mambo ya nje wa Italia Antonio Tajani, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba Italia inaunga mkono vikwazo vipya dhidi ya Tehran, haswa dhidi ya watengenezaji wa droni zilizotumika katika shambulio hilo la wikendi na nyingine zilizorushwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Lebanon, Yemen na katika Ukanda wa Gaza.
Ujerumani yatoa wito wa vikwazo vipya dhidi ya Iran
Katika hatua nyingine kabla ya kuondoka Israel kuelekea Capri hii leo, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock pia alitoa wito wa vikwazo vipya kwa Iran.
Soma pia:Israel yahimizwa kutojibu shambulizi la Iran
Baerbock ambaye ameshawasili Capri amesema kuwa watajadili kuhusu jinsi ya kuzuia kutanuka kwa mzozo huo na kuongeza kuwa kilicho muhimu kwasasa ni kukomesha mashambulizi zaidi kutoka Iran bila ya kuchochea mzozo zaidi.
Ujerumani yataka kuimarishwa kwa ulinzi wa anga wa Ukraine
Baerbock na waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius wametoa wito kwa Umoja wa Ulaya na mataifa wanachama wa jumuiya ya NATO, kuimarisha ulinzi wa anga wa Ukraine haraka iwezekanavyo wakati Urusi ikifanya mashambulizi ya makombora dhidi ya miji yake, suala ambalo pia linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo wa G7.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron, ambaye anatarajiwa kuwasili baadae leo mjini Capri, amesema atashinikiza kuhusu vikwazo vilivyoratibiwa dhidi ya Iran katika mkutano huo wa G7.
Soma pia:Baadhi ya mataifa ya Kiarabu yanaiunga mkono Israe si Iran?
Cameron amedai kuwa Iran inaratibu shughuli nyingi mbaya katika kanda hiyo kuanzia zile zaHamas katika ukanda wa Gaza, Hezbollah kusini mwa Lebanon na waasi wa Houthi nchini Yemen ambao wanahusika na mashambulizi ya meli katika bahari ya Shamu.
Ukraine yaishkuru Ujerumani kwa kuipa mfumo mwingine wa ulinzi wa anga
Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ambaye pia amealikwa kushiriki mkutano huo wa G7 ameishukuru Ujerumani kwa kukubali kuipa nchi yake mfumo mwingine wa ulinzi wa anga aina ya Patriot na kusema atatoa wito kwa mataifa mengine katika mkutano huo wa kuipatia msaada zaidi wa silaha.
Soma pia:Israel yaapa kulipiza kisasi dhidi ya Iran
Kuendelea kutanuka kwa mivutano kati ya Israel na Iran pamoja na vita katika Ukanda wa Gaza na huko Ukraine ni mambo ambayo yatajadiliwa kwenye mkutano huo unaohudhuriwa na mawaziri waMarekani,Uingereza,Ufaransa,Italia,Ujerumani,Canada na Japan na ambao utafanyika kwa siku tatu. Italia ambayo inashikilia nafasi ya uwenyekiti ya kupokezana ya G7 inashinikiza hatua ya kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza pamoja na kumalizwa kwa mivutano katika eneo la Mashariki ya Kati.