Mkutano mrefu wa mazingira wa UN wamalizika bila makubaliano
15 Desemba 2019Baada ya wiki mbili za majadiliano kwa lengo la kupambana na ongezeko la joto duniani, wajumbe kutoka karibu mataifa 200 walipitisha maazimio yanayotoa wito wa kuongeza dhamira kubwa zaidi ya kupunguza gesi zinazosababisha sayari yetu kupata joto zaidi na kuyasaidia mataifa masikini yanayoathirika na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Lakini licha ya kufanya mazungumzo marefu ya mazingira kuwahi kufanyika katika karibu mikutano 25 ya kila mwaka, wajumbe wanaondoka wakiwa wameacha masuala muhimu hadi mkutano ujao mjini Glasgow, mwaka mmoja ujao.
Makundi ya utetezi wa mazingira pamoja na wanaharakati wameyashutumu mataifa tajiri kwa kuonesha dhamira ndogo ya kupambana kwa dhati na mabadiliko ya tabia nchi.
Masoko ya gesi za kaboni yameweka bei kwa utoaji wa gesi za kaboni dayoksaidi, gesi ambayo inaharibu mazingira, na kuruhusu mataifa ama makampuni kuuza utoaji wa gesi hizo ambazo zinaweza taratibu kupunguzwa, na kuhimiza matumizi ya teknolojia zinazotoa gesi hizo chafu kwa kiwango kidogo.
Mataifa ya Ulaya na kwingineko yamesema kuwa kukosekana kwa makubaliano juu ya kushughulikia mabadilishano ya mikopo ya gesi za kaboni ni bora kuliko kuwa na makubaliano dhaifu ambayo yanaweza kudhoofisha taratibu dazeni kadhaa ama zaidi zilizopo kikanda.
Maandamano ya hasira
"Kwa bahati nzuri, sheria dhaifu katika soko chini ya misingi ya utaratibu, unaopigiwa upatu na Brazil na Australia, ambao ungedhoofisha juhudi za kupunguza utoaji wa gesi hizo chafu, umewekwa kando," amesema Mohamed Ado, mkurugenzi wa Power Shift Africa, kundi linalofanya kampeni.
Mazungumzo kwa wakati fulani yaliandamana na maandamano ya hasira kutoka kwa makundi ya watu wa asili na makundi ya mazingira, ndani na nje ya ukumbi wa mkutano. Waandamanaji wameakisi hali ya kukata tamaa inayoendelea, hususan miongoni mwa vijana, kuhusu kasi ndogo sana ya juhudi za serikali kuzuwia mabadiliko ya tabia nchi.
Miongoni mwa nyaraka ambazo mkutano huo wa Umoja wa mataifa umepitisha leo Jumapili (15.12.2019) ni azimio la "Muda wa kuchukua hatua Chile-Madrid" likitoa mwito wa mataifa kuimarisha ahadi zao za hivi sasa za kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira. Hii inahitajika kuwa katika msitari pamoja na malengo ya makubaliano ya Paris ya 2015 ya kuepuka ongezeko la nyuzi joto zaidi ya 1.5 'Celsius' ifikapo mwishoni mwa karne hii.
Hadi sasa, dunia imo njiani kufikia ongezeko la nyuzi joto 3 hadi 4, kukiwa na uwezekano wa matokeo mabaya zaidi kwa nchi nyingi.
Mataifa pia yamekubaliana kuweka fedha kwa mataifa ambayo yamo katika hatari zaidi na yasiyo na uwezo kuwapa fidia kwa ajili ya athari za matukio ya hali mbaya ya hewa, moja kati ya masuala ya dharura zaidi kwa mataifa madogo ya visiwani.