Mkutano mkuu wa kanisa katoliki dhidi ya ubakaji magazetini
25 Februari 2019Tunaanzia Vatican ambako kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni, Papa Francis aliufunga mkutano mkuu wa aina yake uliojadili namna ya kukabiliana na balaa la kunajisiwa watoto na mapadri kanisani. Hotuba yake iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu haikumridhisha kila mmoja linaandika gazeti la "Schwäbische Zeitung":"Hali ya kuvunjika moyo, hasira, na hali ya kukata tamaa": Hisia zilizojitokeza kufuatua hotuba ya Papa Francis zinabainisha kwamba kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni, anaetokea Argentina anaweza kujikuta njia panda. Anaweza kujikwaa katika vigezo alivyoviweka mwenyewe. Kwanini anawanyeshea kidole wengine. Kuungama, unyenyekevu, toba ndio vinavyohitajika.
Matokeo ya mkutano mkuu wa kanaisa katoliki hayatoshi hata kidogo
Bila ya shaka mkutano wa kilele dhidi ya desturi za udhalilishwa watoto kingono ulikuwa muhimu lakini umekawia kuitishwa. Matumaini yalikuwa makubwa: baada ya miaka yote iliyopita, ambapo mengi yalisemwa, machache yaliyotendeka, kanisa lingeonyesha hivi sasa limedhamiria kikamilifu. Matokeo yangebidi yawe: Mapadri waliowadhalilisha watoto wanafukuzwa na kuadhibiwa. Kadhia zao zinakabidhiwe waendesha mashitaka. Maaskofu wanaoficha kinachotokea na wao pia wapokonywe kazi. Lakini badala yake Papa anatangaza kuunda tume na kuratibu muongozo-hayo hayatoshi hata kidogo."
Kitisho cha kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe Venezuela
Mzozo wa Venezuela unazidi makali. Machafuko ya mwishoni mwa wiki yamepelekea watu kuuwawa na wengine kujeruhiwa. Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linaandika:"Kinyang'anyiro cha kuania madaraka kati ya rais Nicolas Maduro na rais aliyejitangaza mwenyewe wa mpito Juan Guaido kimezidi makali. Baada ya rais Maduro kuigeuza nchi yake kuwa ngome na kuzuwia misaada ya dharura inayohitajika, hatima inaonyesha kuwa ni moja tu: umwagaji damu. Ama wananchi wananyanyuka na kuasi au hujuma zinatoka nje. Siku za Maduro kama rais zinakurubia mwisho wake. Anamtaja rais wa mpito Juan Guaido kuwa karagosi. Lakini na yeye mwenyewe pia si bora. Sababau pekee kwanini Maduro bado anaranda ni jeshi. Maafisa wanahofia mageuzi. Na hao ndio Guaido anaowategemea. Hadi wakati huu wanajeshi 60 tu ndio waliotoroka na kujiunga na upande wa upinzani na sio jeshi lote.
Mkutano mkuu wa chama cha die Linke wamalizika bila ya matokeo
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mkutano mkuu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto die Linke uliomalizika jana mjini Bonn. Gazeti la "Die Welt" linaandika: Katika nukta moja chama cha die Linke kinastahiki sifa: utaratibu wao wa kujadiliana chamani ni wa kupigiwa mfano katika medani ya vyama vya kisiasa nchini Ujerumani. Lakini hata wafuasi wa die Linke wanabidi mwishoni mwa mikutano yao wafikie maamuzi pia.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Khelef