1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu nafasi za juu za Umoja wa Ulaya waahirishwa

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
1 Julai 2019

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameahirisha mkutano wa kutafuta watakaochukua nafasi za juu za uongozi wa Umoja huo. Mkutano huo utaendelea tena Jumanne mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/3LQ0N
EU-Gipfel in Brüssel | Emmanuel Macron, Donald Tusk & Angela Merkel
Picha: Getty Images/AFP/K. Tribouillard

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk ambaye anaongoza mazungumzo hayo amesema watakutana tena hapo kesho kuendelea na mchakato wa kumtafuta atakayemrithi Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker anayeondoka.

Hatua hiyo inahitaji idhini ya viongozi 21 kati  ya 28 wa Umoja wa Ulaya, wanaowakilisha asilimia 65 ya wakazi wa umoja huo na mara baada ya viongozi hao wa Umoja wa Ulaya kuwateua wagombea, watapaswa kupitishwa na Bunge la Ulaya.

Kaimu Kansela wa Austria Brigitte Bierlein amesema zoezi la kugawa nafasi hiyo za juu katika Umoja wa Ulaya lilishindikana kutokana na ukosefu wa kuzingatia usawa.

Makamu wa Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Frans Timmermans
Makamu wa Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Frans TimmermansPicha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Makamu wa Rais wa sasa wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Frans Timmermans  raia wa Uholanzi, ambaye alikuwa Mgombea wa chama chama  S/D katika uchaguzi wa mwezi Mei wa bunge la Ulaya, alikua ndio mwenye nafasi nzuri kuchukua wadhfa wa Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya.  

Kristalina Georgieva wa Bulgaria alitazamiwa kupewa wadhfa wa Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya na hivyo kumrithi Donald Tusk. Wengine waliokuwa katika mstari wa mbele wa kupata nyadhfa hizo za juu ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ubelgiji Charles Michel na Kamishna wa ushindani wa Umoja wa Ulaya Margrethe Vestager kutoka Denmark ambaye alitazamiwa kuchukua nafasi ya mkuu wa sera za Mambo ya Nje wa umoja wa Ulaya.

Bwana Timmermans alikuwa chaguo la makubaliano kati ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel walipokutana pembezoni mwa mkutano wa G20 huko Japan, ambapo pia makubaliano hayo yalijumuisha nafasi zingine za juu katika Umoja huo. Makubaliano hayo pia yaliungwa mkono na Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez.

Miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zimeripotiwa kumpinga  Frans Timmermans ni Poland, Hungaria, Jamhuri ya Czech, Croatia, Slovakia na Ireland.

Chama cha kihafidhina cha (EPP), kilichoongoza kwa kupata viti vingi katika uchaguzi wa bunge la Ulaya, hakikukubali kusalimu amri  kimeendelea kumuunga mkono kwa mgombea wao, mjumbe  wa Ujerumani Manfred Weber.

Waziri Mkuu wa Ireland Leo Varadkar aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumapili kwamba haitakuwa rahisi kwa mawaziri wakuu wa muungano wa vyama vya EPP kukubali kuachia nafasi ya Urais wa haalmashauri ya Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban alipeleka barua ya onyo kwa wanachama wa EPP kwamba uteuzi wa Timmermans utakuwa makosa makubwa yatakayoingia kwenye historia.

Taasisi za Umoja wa Ulaya zinatakiwa kuwakilisha maslahi ya mataifa yote wanachama katika ngazi ya kimataifa na kwenye makao makuu mjini Brussels.

Vyanzo: https://p.dw.com/p/3LNIm/DPAE/RTRE