Mkutano kuhusu mzozo wa Ukraine wafanyika Geneva
17 Aprili 2014Mawaziri wa masuala ya nchi za nje wa Marekani, Urusi, Ukraine na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Geneva hii leo, katika juhudi za kutafuta suluhu kwa mzozo wa Ukraine. Mazungumzo hayo ya mjini Geneva yameanza kwa mkutano uliowaleta pamoja waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry, na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton. Baadaye wanadiplomasia hao wanategemewa kukaa meza moja na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov, na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ukraine, Andrii Deshchytsia.
Kabla ya mkutano huo, wanadiplomasia wa nchi za magharibi wamesema hawatarajii kupatikana kwa muafaka wowote, kwa kuzingatia pengo kubwa lililopo kimsimamo kati ya Urusi na pande nyingine tatu katika mazungumzo, hususan kuhusu hatua ya Urusi ya kulichukua jimbo la Crimea kutoka Ukraine, na mchango wake katika ghasia zinazoendelea mashariki mwa Ukraine, ambako wakazi wengi wanazungumza lugha ya kirusi.
Ajenda muhimu katika mazungumzo ya Geneva ni kujadili namna ya kupunguza mvutano, kuwanyang'anya silaha wanaharakati, mabadiliko ya katiba ya Ukraine pamoja na uchaguzi unaotarajiwa kufanywa katika nchi hiyo. Nchi za magharibi hali kadhalika zinaitaka Urusi kuondoa maelfu ya wanajeshi wake ambao inasemekana wamerundikwa karibu na mpaka wa Ukraine.
Ujumbe wa Ukraine katika mazungumzo hayo unategemewa kutoa mapendekezo juu ya namna ya kuyashughulikia matakwa ya wakazi wa mashariki wanaozungumza kirusi, na wakati huo huo kuonyesha ushahidi ilio nao, kuthibitisha ushirikiano kati ya Urusi na wanaharakati wanaotaka kujitenga.
Shinikizo lazidi dhidi ya Urusi
Muda mfupi kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo mjini Geneva nchi za magharibi zimezidisha shinikizo dhidi ya Urusi. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney alisema jana kuwa serikali ya nchi hiyo ilikuwa tayari kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi, na kwamba mkutano huu ungeonyesha kama Urusi inayo azma ya kupunguza mvutano au la.
Wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea mjini Geneva, taarifa ya wizara ya mambo ya ndani ya Ukraine imesema wanajeshi wa nchi hiyo wamewauwa wanaharakati 3 wanaoiunga mkono. Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Arsen Avakov amesema watu wapatao 300 walikivamia kituo cha kijeshi cha Mariupol usiku wa kuamkia leo, na kuwashambulia walinzi kwa risasi na mabomu ya petroli.
Waziri huyo ameongeza kuwa walinzi hao walijibu mashambulizi, na kwa kushirikiana na kikosi maalum pamoja na helikopta waliweza kuwafukuza wanaharakati hao, na kuwakamata 63 miongoni mwao. Msemaji wa wanaharakati hao ambao wanaiunga mkono Urusi amesema kuwa watu hao waliokishambulia kituo cha Mariupol hawakuwa wenyeji wa mahali hapo.
Na kuhusiana na mzozo huo huo wa Ukraine, Rais wa Urusi Vladimir Putin amekiri kwa mara ya kwanza kwamba wanajeshi wa nchi yake walikuwa katika jimbo la Crimea, kabla na wakati wa kura ya maoni iliyosababisha kujitenga kwa jimbo hilo na Ukraine na kujiunga na Urusi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/DPAE/AFPE
Mhariri: Josephat Charo