1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa Urafiki kati ya Ujerumani na Ufaransa

Oumilkheir Hamidou
22 Januari 2019

Mkataba mpya wa urafiki kati ya Ujerumani na Ufaransa , hatima ya makubaliano ya Brexit, na kongamano la kimataifa la kiuchumi huko Davos ni miongoni mwa mada zilizomulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/3BwyQ
Belgien, EU-Gipfel - Emmanuel Macron, Präsident von Frankreich und Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: Getty Images/E. Dunand

 Tunaanzia katika mji wa mpakani wa Aachen ambako kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanatia saini mkataba mpya wa urafiki kati ya nchi zao, miaka 56 baada ya mkataba kama huo uliotiwa saini katika kasri la Elysée. Gazeti la Schwäbische Zeitung linajiuliza :"Eti kweli Ujerumani na Ufaransa zinahitaji mkataba mpya wa urafiki? Kwani mkataba wa Elysée uliotiwa saini mwaka 1963 si unazingatia yote yale ambayo "mahasimu hao wakubwa wa zamani" wanayahitaji mpaka leo. Ni waraka wa suluhu wa kihistoria na usiokuwa na kikomo ambao  Charles de Gaulle na Konrad Adenauer wamefanikiwa kuutia saini baada ya vita vitatu kati ya nchi zao. Na Emmanuel Macron na Angela Merkel je? Ni kweli kwamba Merkel alimpa kisogo kidogo Macron baada ya hotuba yake kuhusu sera za Umoja wa ulaya.

Mkatba wa urafiki kati ya Ujerumani na Ufaransa ni muhimu sanaa wakati huu

Ni kweli pia kwamba mkataba wa Aachen haukukidhi matarajio yote. Lakini kwamba umeweza kutia saini, hilo pekee linatosha. Na hasa katika enzi hizi ambazo rais wa Marekani Donald Trump anafikiria uwezekano wa kujitoa katika jumuia ya kujihami ya NATO. Katika wakati huu ambao Waingereza wanaelekea kujitoa katika Umoja wa ulaya bila ya makubaliano na pia katika wakati huu ambao wafuasi wa siasa kali za kizalendo wanazidi kupata nguvu barani Ulaya. Huu hasa ndio wakati ambao Ujerumani na Ufaransa wanabidi kuwajibika dhidi ya Marekani na yeyote yule anaedhamiria kuuvunja Umoja wa Ulaya."

Hatima ya Brexit ikoje?

Hatima ya makubaliano ya kujitoa Uingereza katika Umoja wa ulaya nayo pia imemulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika:"Waziri mkuu Theresa May haangaliwi tena na Umoja wa Ulaya kama mshirika, badala yake anazingatiwa zaidi kama tatizo katika mazungumzo kati ya pande mbili zinazopakana na ujia wa maji. Nyumbani hakufanikiwa kupata ridhaa inayojumuisha pande zote. Na mjini Brussels nanga zinapaa. Ni shida kwa namna hiyo kuashiria vipi waziri mkuu huyo anaweza kujiandaa kuitoa nchi yake katika umoja wa Ulaya kwa njia zinazofaa."

Ulaya yakodolea macho yanayotokea katika bahari ya kati

Na hatimae gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" limeandika kuhusu kongamano la kiuchumi la Davos likizingatia zaidi suala la uhamiaji. Gazeti linaendelea kuandika:"Kuna mada inayostahiki kwa kila hali kujadiliwa: Njia wanayopitia wakimbizi katika bahari ya kati. Ulaya inakodoa macho tu, miaka mitatu baada ya balaa la mamia ya watu kuzama katika bahari ya kati.Mpaka sasa bado hakuna makubaliano ya maana yaliyotiwa saini pamoja na Libya ambako wengi wanamalizikia katika kambi za kuwakusanya wahamiaji; wala hakuna mradi katika nchi wanakotokea ili kupaambana na chaanzo cha ukimbizi.Ulaya inafanya yale yale yaliyoshuhudiwa na matokeo yake tunayajua."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Gakuba, Daniel