Mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi umepatikana
13 Desemba 2015Makubaliano hayo yatakayotekelezwa ndani ya miongo kadhaa ni katika juhudi za kuzuwia ongezeko la ujoto duniani.
Baada ya miaka minne ya mapambano katika mazungumzo ya Umoja wa Mataifa mara kadhaa yakiwa baina ya maslahi ya nchi tajiri dhidi ya nchi masikini, mataifa ya visiwani yaliyoko katika hatari dhidi ya mataifa yanayoinukia kiuchumi, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius alitangaza kuidhinishwa kwa makubaliano hayo, akishangiliwa na wajumbe kutoka karibu mataifa 200 duniani.
"Kwa nyundo ndogo unaweza kufanikiwa katika mambo makubwa," Fabius amesema wakati akithibitisha kufikiwa makubaliano hayo, akikamilisha wiki mbili za majadiliano makali katika mkutano huo nje kidogo ya mji mkuu wa Ufaransa, Paris.
Ni ushindi kwa wote
Yakimwagiwa sifa kama makubaliano halisi ya mabadiliko ya tabia nchi duniani, yakiyapa jukumu nchi tajiri na masikini kuzuwia ongezeko la utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira zinazolalamikiwa kwa kuleta ujoto duniani, mkataba huo umeweka malengo ya haraka, ya muda mrefu ya kutokomeza kabisa utoaji wa gesi zinazotengenezwa na binadamu zinazoharibu mazingira katika karne hii.
"Ni ushindi kwa wote katika sayari hii pamoja na vizazi vijavyo," amesema Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, John Kerry ambaye aliongoza majadiliano kwa upande wa Marekani katika mazungumzo hayo ya Paris.
Nae rais wa Marekani Barack Obama , amesema makubaliano ya mabadiliko ya tabia nchi "yanatoa fursa nzuri kuiokoa sayari pekee tuliyonayo" na ameusifu utawala wake kuwa ulikuwa ni nguzo kuu ya kupatikana makubaliano hayo.
Obama akizungumza usiku wa jana Jumamosi katika Ikulu ya Marekani ya White House, alisherehekea kile ambacho kinaweza kuwa mafanikio muhimu yatakayodumu - iwapo baraza la Congress la Marekani linalodhibitiwa na chama cha Republican ama mahakama hazitamzuwia yeye binafsi ama mrithi wa kiti chake katika Ikulu ya Marekani kubadilisha yaliyofikiwa.
Wabunge wapuuzia makubaliano hayo
Obama amesema makubaliano hayo sio kamili, lakini yanaweka utaratibu ambao utafanya mapitio kwa vipindi mbalimbali pamoja na tathmini kuhakikisha kwamba nchi zinatimiza majukumu yao ya kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira.
Wabunge wa ngazi ya juu wa chama cha Republican hata hivyo wanapuuzia makubaliano hayo kuwa hayana chochote zaidi ya kwamba ni waraka wa muda mrefu wa mipango na kusema Obama anatoa ahadi ambazo hataweza kuzitimiza. Wamesema nia yake ya kupunguza utoaji wa gesi kutoka kwa viwanda vya kuzalisha nishati nchini Marekani itapoteza maelfu ya nafasi za ajira kwa Wamarekani na kupandisha gharama za umeme.
Makubaliano hayo ya kabla ya mwaka 2020 ya mjini Paris yanamaliza mivutano ya miongo kadhaa baina ya mataifa tajiri na masikini kuhusiana na vipi kutekeleza kile kitakachokuwa kampeni ya mabilioni ya dola kuzuwia ongezeko la ujoto duniani na kuweza kumudu athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Kutokana na uchunguzi kwamba mwaka 2015 ulikuwa na joto kali zaidi kuwahi kuorodheshwa, viongozi wa dunia pamoja na wanasayansi wamesema makubaliano hayo ni muhimu kwa kuthibiti kupanda kwa ujoto na kuepusha athari mbaya zaidi katika mabadiliko ya tabia nchi.
Mwandishi: Sekione Kitojo/AFPE, APR,RTRE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo