1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Mjumbe wa RSF asema ni wakati wa amani Sudan, Darfur

25 Julai 2023

Mjumbe mkuu wa wanamgambo wa msaada wa dharura - RSF amesema kuwa ni wakati wa kuleta amani nchini Sudan na jimbo la Darfur katika wakati vita vya RSF na jeshi la Sudan vikifikisha siku yake ya 100

https://p.dw.com/p/4ULD1
FILE PHOTO: A Sudanese national flag is attached to a machine gun of Paramilitary Rapid Support Forces (RSF) soldiers as they wait for the arrival of Lieutenant General Mohamed Hamdan Dagalo before a meeting
Picha: Umit Bektas/REUTERS

Ezzat amesema mjini Lome, wako tayari kushiriki aina yoyote ya mkutano wa amani na kuwaleta pamnoja watu na kusitisha vita. "Sote tunatafuta amani. Watu wa Sudan wanatafuta amani. Watu wa Sudan wanateseka kutokana na vita kwa miongo mingi katika majimbo kama Darfur, Blue Nile, Sudan Kusini na Sudan Mashariki na sasa katika mji mkuu Khartoum. Kwa hiyo huu ndio wakati wa kusitisha vita na kuanzisha mustakabali mpya kwa watu wa Sudan, amani, maendeleo, haki na usawa."

A view shows a damaged building as clashes between the army and the paramilitary Rapid Support Forces (RSF) continue, in Omdurman
Vita vya Sudan vimefikisha siku 100 tangu kuanza Aprili 15Picha: Mostafa Saied/REUTERS

Vita vya Sudan vilizuka katika mji mkuu Khartoum Aprili 15 na kusambaa hadi Darfur, ambapo karibu watu 3,000 wameuawa kote nchini humo na mamia kwa maelfu kuyakimbia makazi yao.

Vita hivyo vinawakutanisha mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan dhidi ya naibu wake Mohamed Hamdan Dagalo, kamanda wa wanamgambo wa RSF.

Nouri Abdalla, kutoka kundi muhimu la waasi jimboni Darfur, amesema mazungumzo ya Togo yanalenga kutengeneza ramani ya kukomesha machafuko Darfur na kwingineko.

Amesema mkutano huo wa Lome pia ulijadili mbinu za kufungua upya uwanja wa ndege wa El-Geneina chini ya udhibiti wa RSF, ili kuruhusu upelekaji wa misaada ya kiutu.

Na wakati RSF wakitoa ujumbe wa kupatikana amani, jenerali mmoja wa jeshi la Sudan amepinga kwa kutumia lugha ya vitisho pendekezo linaloongozwa na Kenya kuwa wanajeshi wa kulinda amani wa Afrika Mashariki waingilie kati vita hivyo. Kauli za jenerali hiyo zimezusha ukosoaji mkali kutoka kwa maafisa nchini Kenya.

Mzozo wa wakimbizi wa Sudan

Mapema mwezi huu, jumuiya ya maendeleo ya kikanda IGAD ambayo Kenya ni mwanachama, ilipendekeza mpango ambao ungejumuisha kupelekwa walinda amani mjini Khartoum.

Jeshi la Sudan limekataa mara kwa mara mpango huo unaoongozwa na Kenya, likiituhumu nchi hiyo kwa kuwaunga mkono RSF. Linasema litawachukulia walinda amani wowote wa kigeni kuwa maadui wao. Jenerali wa Sudan Yassir al-Atta amesema na hapa namnukuu "Viacheni vikosi vya Afrika Mashariki pale vilipo. Lileteni jeshi la Kenya. Naapa kwa jina la Mungu, hakuna hata mmoja wao atakayerejea kwao,” mwisho wa kumnukuu.

Katibu Kiongozi katika Wizara ya Mambo ya Kigeni nchini Kenya Korir Sing'Oei amesema taarifa hiyo haifai kupata jibu lolote kutoka kwa serikali. Amesema tuhuma hizo hazina msingi, na kuwa nchi yake haiegemei upande wowote.

AFP, AP