Mjumbe maalum wa UN aitaka Marekani kumaliza vita Syria
25 Novemba 2016Urusi haitaki kubebeshwa jukumu la kuharibiwa kwa eneo la mashariki la Aleppo na wakati huo huo mkuu wa kundi la kujitolea la "White Helmets" amesema wakaazi waliozingirwa mjini Aleppo wana siku kumi tu kabla ya kuanza kufa kwa njaa.
"Siwezi kumdharau rais wa Marekani anayeondoka madarakani kuwa hana nguvu tena," Staffan de Mistura mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Syria alisema katika mahojiano yaliyochapishwa leo katika gazeti la Ujerumani la Sueddeutsche Zeitung.
"Rais Obama , na waziri wake wa mambo ya kigeni John Kerry wana nia ya kumaliza msiba mkubwa wa kibinadamu katika karne hii ambao umekuwao katika wakati wa uongozi wao. Ni suala litakalobaki katika muda wao wa uongozi," amesema de Mistura.
De Mistura siku ya Jumanne alieleza wasi wasi wake kwamba rais wa Syria Bashar al-Assad anaweza kuanzisha mashambulizi mpya ya kinyama kuwasambaratisha waasi wanaolishikilia eneo la mashariki mjini Aleppo kabla ya rais mteule wa marekani Donald Trump kuingia madarakani Januari 20.
Amesema mkutano wake wa hivi karibuni mjini Damascus ulionesha serikali ya Syria imetiwa moyo na matamshi ya Trump wakati wa kampeni za uchaguzi kuhusiana na kuacha kuwaunga mkono wapinzani nchini Syria. Lakini amesema aliwakumbusha viongozi wa Syria kwamba rais yeyote wa Marekani atakabiliwa na mbinyo mkubwa wa umma iwapo hali inafikia katika maafa ya kiutu ambapo watu 200.000 wanakabiliwa na njaa.
Watu wanapungua kutokana na vifo Aleppo
De mistura amesema anahofia idadi ya watu Aleppo mashariki inaweza kupungua ifikapo wakati wa Krismasi iwapo mashambulizi ya mabomu yataendelea, hali ambayo inaweza kuwalazimisha maelfu ya wakimbizi kukimbilia Uturuki, na kusababisha vita vya muda mrefu vya chini kwa chini katika maeneo ya vijijini na mashambulizi ya mabomu katika magari mijini.
Mkuu wa kundi la kujitolea nchini Syria linalojulikana kama "White Helmets" Raed al Saleh amesema jana wakaazi waliozingirwa mjini Aleppo wana siku kumi tu kabla ya kukabiliwa na kifo kwa njaa.
"Tatizo tunalokumbana nalo White Helmets , ni kwamba vituo vyetu mjini Aleppo vimeshambuliwa na sasa tunafanyakazi kama nilivyokuambia , na vifaa tulivyoweka kama vya msaada na vifaa ambavyo tumeweza kuvipata kutoka katika vifusi , na vifaa ambavyo havikuharibiwa. Nafikiri kundi la White Helmets, kwa mujibu wa taarifa nilizonazo, linaweza kuendelea kwa mwezi mmoja kuwasaidia watu walioko katika vifusi, hata hivyo hatutoi matibabu ya upasuaji kama madaktari wanavyofanya na nafikiri hili ni tatizo katika hospitali hivi sasa, kwa wale waliojeruhiwa. Tunaweza kuhudumia kwa muda wa mwezi mmoja tu."
Pamoja na hayo amesema anaamini kwamba Urusi haitaki kabisa kubebeshwa lawama kwa kuharibiwa kwa Aleppo mashariki. Wakati huo huo raia 32 , ikiwa ni pamoja na watoto watano, wameuwawa jana katika mashambulizi ya anga ya jeshi la serikali dhidi ya eneo la mashariki la mji wa Aleppo linalodhibitiwa na waasi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Yusra Buwayhid