Mji wa kwanza Ujerumani wakaazi wake wazuiwa kutoka nje
20 Machi 2020Wakaazi wake wametakiwa kubakia nyumbani kutokana na hali inayozidi kuwa mbaya ya kusambaa kwa virusi vya Corona.
Wakaazi 6,500 wa mji huo wamekatazwa kutoka majumbani mwao bila sababu maalum, hali ambayo inaonekana kuwa ndio kitu kinachokaribia kutokea kwa nchi nzima ambako watu wengi wamekaidi hatua za kubakia nyumbani. Wakaazi wa mji huo wa Mitterteich, ulioko katika wilaya ya Tirschenreuth kusini mwa jimbo la Bavaria , waliamka leo wakishuhudia aina nyingine ya maisha.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya hiyo Wolfgang Lippert , wakaazi wanaweza kutoka tu majumbani mwao iwapo wanakwenda kazini , kumuona daktari ama wanakwenda kununua mahitaji yao.
Lakini pia inaonekana wakaazi hao wanaikubali hali hiyo. "Ni vizuri kwamba huu ni mji wa kwanza kuwekewa amri hiyo ya kutotembea ovyo, na ni vizuri kwamba inafanyika kwa msisitizo mkubwa," mkaazi wa eneo hilo Sandra Wedlich amesema.
Hatua hizo zimechukuliwa baada ya mji huo wa Mitterteich kujitokeza kuwa eneo la hatari la virusi vya Corona, kwa kuwa na watu karibu 40 ambao wameambukizwa virusi hivyo katika wilaya ya Tirschenreuth. Maafisa wanaamini kuwa mengi ya maambukizi yanahusishwa na sherehe za hivi karibuni za unywaji bia.
Jimbo la Bavaria ni moja kati ya majimbo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa nchini Ujerumani, kwa mujibu wa tarakimu rasmi kutoka katika taasisi ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch. Lakini maambukizi yanasambaa haraka kwingineko, na kusababisha kansela Angela Merkel kutoa wito kwa wananchi katika hotuba yake kupitia televisheni siku ya Jumatano jioni kuwa wapunguze mikusanyiko ya kijamii.
Ujerumani imeripoti ongezeko la siku moja la zaidi ya maambukizi 2,800 kufikia jana, na kufanya idadi jumla ya watu walioambukizwa virusi vya Corona kufikia 10,000.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer amesema ikiwa hali itakuwa mbaya zaidi , basi jeshi litatumika katika kupambana na virusi hivyo kutokana na kuwa na nyenzo stahili.
"Wote tunatambua kuwa mapambano dhidi ya virusi vya corona ni ya muda mrefu. Mwishoni, tutatokeza katika barabara ndefu ambayo itatupatia njia ya kuwa na vifaa. Hilo litakuwa jukumu mahsusi la jeshi la Ujerumani. Ndio sababu bado hatujachukua hatua kama ilivyo kwa huduma nyingine za jamii kwa wakati huu. Hata hivyo tunajitayarisha kwa vifaa na ikitokea kwamba huduma za kijamii zinafikia ukomo, jeshi la Ujerumani na vifaa vyake litakuwa tayari."
Mipaka imefungwa nchini Ujerumani kuzuwia janga hili, wakati nchi nzima maduka yamefungwa, migahawa imelazimika kufanyakazi kwa muda maalum na watu wametakiwa kufanyakazi kutokea nyumbani.