Mjadala waibuka kuhusu mageuzi ya katiba nchini Uganda
7 Januari 2022Joto lingine la kubabadili katiba ya Uganda linafukuta wakati ambapo wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi wakipendekeza kuwa rais achaguliwe na wabunge badala ya raia wenyewe moja kwa moja kama ilivyo sasa. Kulingana na wale wanaopigia debe wazo hilo, hii itahakikisha amani na utulivu wakati wa uchaguzi na upinzani hautadai kwamba udanganyifu umetokea.
Felix Adupa ambaye ni kiongozi wa kundi la NRM Transfomer Cadres amefafanua hivi kuhusu uzuri wa wabunge kumchagua rais badala ya wananchi.
Wale wanaounga mkono wazo hilo wanaelezea kuwa uchaguzi wa rais hugharimu taifa kiasi kikubwa cha pesa na Uganda ingejifunza kutoka kwa mataifa mengine ambayo hufuata mfumo huo kama vile Canada.
Upinzani walalamikia njama ya NRM
Lakini wanasiasa wa upinzani pamoja na watu mbalimbali ikiwemo vijana wana mtazamo kuwa hii ni hila ya kumwezesha rais Museveni kuweza kuendelea kutawala baada ya kukumbwa na ushindani mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2021 katika kinyang'anyiro ambapo mgombea Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine alileta ushindani mkali.
Kulingana na mchambuzi na mwanahabari Abdusalam Waiswa, itakuwa rahisi kwa wabunge wa chama tawala kushawishiwa chini ya mfumo kama huo.
Kwa sasa, idadi kubwa ya wabunge ni kutoka chama cha NRM wakijumuisha zaidi ya asli mia 90. Hii ina maana kuwa ikiwa muswaada huo utafaulu kufikishwa bungeni na waridhiane nao, basi itakuwa rahisi kwa rais Museveni kuongoza Uganda kwa awamu nyingi bila wasiwasi wowote.