1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yaomba misaada zaidi kuingia Gaza kwa njia za ardhini

14 Machi 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry ametoa wito wa kuongezwa kwa misaada ya kiutu kuelekea Gaza kupitia njia za ardhini, licha ya msaada wa tani 200 kuwa njiani kuelekea Gaza kutoka Cyprus kwa njia ya bahari.

https://p.dw.com/p/4dWjK
Misri | Sameh Shoukry
Waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry Picha: Mohamed Abd El Ghany/REUTERS

Shoukry amesema watu aliokata tamaa huko Gaza hawawezi kusubiri hadi bandari ya muda itakayotengenezwa na Marekani itakapokamilika kwa ajili ya kupokea misaada kwa njia ya bahari.

Hayo yakiarifiwa Israel inasema inapanga kuwaambia Wapalestina milioni 1.4 katika mji wa kusini wa Rafah, watafute hifadhi huko Gaza ya kati, kuelekea mpango wake kufanya mashambulizi ya kijeshi eneo la kusini.

Msaada taratibu unaingia Ukanda wa Gaza japo Israel inaendelea na mashambulizi katika eneo hilo.

Israel inasema hamas bado ina vikosi vinne vya kijeshi huko rafah, inavyotaka kuvisambaratisha.

Wakati huo huo, wizara ya afya ya Palestina inayoendeshwa na wanamgambo wa Hamas imesema mashambulizi ya Israel leo yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 31,000 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 73,000.