Misri yamwachia huru mwanaharakati kinara wa demokrasia
19 Agosti 2023Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi ametoa msamaha kwa wafungwa kadhaa akiwemo mwanaharakati maarufu anayedai demokrasia Ahmed Douma.
Douma alikuwa kinara wakati wa vuguvugu la umma nchini Misri mwaka 2011, ambalo lilichangia Rais wa muda mrefu Hossein Mubarak kujiuzulu. Mwanaharakati huyo, ambaye sasa ana umri wa miaka 37, alizuiliwa mara kadhaa chini ya utawala wa Mubarak na baada ya rais huyo kuangushwa.
Mnamo mwaka 2015, mahakama ya Misri ilimhukumu Douma kifungo cha maisha jela, kwa mashtaka ya kuvishambulia vikosi vya usalama na kuharibu majengo ya serikali wakati wa maandamano ya ghasia zaidi ya miaka mitatu iliyopita. Mamia ya viongozi wa upinzani na wanaharakati wamezuiliwa tangu wakati huo na kuhukumiwa kifungo jela, lakini sasa wanaachiwa huru chini ya msamaha wa rais.