Misri yakata tiketi ya kucheza AFCON 2024
15 Juni 2023Timu ya taifa ya Misri imepata ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Guinea katika mtanange uliopigwa hapo jana na kujikatia tiketi ya kushiriki kwa mara ya 26 mfululizo michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON. Ushindi huo unaifanya Misri kuwa taifa la nane kufuzu kushiriki michuano hiyo ya bara zima itakayofanyika nchini Code d'Ivoire mwaka ujao ikijumuisha timu 24. Magoli ya washambuliaji wawili Mahmoud Trezeguet na Mostafa Mohamed ndiyo yaliiwezesha Misri kuongoza kundi D na kufungua milango ya kushiriki michuano AFCON. Misri imewahi kutwaa taji la mabingwa wa Afrika mara saba tangu mashindano ya AFCON yalipoanzishwa. Timu ya taifa ya Guinea ilihitaji alama moja tu kukata tiketi ya AFCON, lakini kichapo cha hapo jana kimetia kiwingu nafasi hiyo.