Misri yaanza maandalizi ya AFCON 2019
14 Januari 2019Achraf Sobhi ni Waziri wa michezo. "kutakuwa na kamati kuu itakayoongozwa na Waziri Mkuu, na kuwajumuisha mawaziri wote wanaohusiana na mashindano hayo, ili kulifanikisha jukumu la Shirikisho la soka.
Sobhi pia amesema hafla ya ufunguzi na mechi ya kwanza vitafanyika kwenye uwanja wa taifa wa Cairo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 74,000, ambao ulifanyiwa matengenezo kabla Misri haijawa mwenyeji wa michuano ya mwaka 2006.
Waziri mkuu wa Misri, Moustafa Madbouli amesema mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba tayari wameanza kuurekebisha uwanja huo, huku rais wa shirikisho la soka Hany Abou Rida akisema wana imani watashinda kombe hilo. "kuandaa mashindano hayo katika miezi mitatu au minne ni ishara nzuri ya imani kutoka kwa rais wa FIFA Infantino, na wenzangu katika CAF. Misri ilipata kura 16 dhidi ya moja kumaanisha wengi wana Imani kuhusu Misri na uchumi wake.
Wiki iliyopita, Misri ilichukua nafasi hiyo ya kuwa mwenyeji wa michuano ya mwaka huu wa 2019 baada ya Cameroon kunyang'anywa zabuni kutokana na kucheleweshwa kwa ujenzi wa miundombinu na hali tete ya kisiasa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Iddi Ssessanga