Misaada ya dharura ya Marekani imekwama mpakani Venezuela
8 Februari 2019Malori mawili yaliyojaa chakula cha msaada na madawa yaliwasili katika mpaka wa Colombia katika mji wa Cucuta, ambao uko upande wa pili wa mto kutoka Venezuela.
"Marekani inaleta bidhaa, ikiwa ni pamoja na chakula, vyakula vya ziada vya virutubishi mwilini, bidhaa za usafi pamoja na madawa, nchini Colombia ili viweze kuwafikia wale wenye uhitaji nchini Venezuela , haraka iwezekanavyo," amesema afisa wa Marekani , akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwasababu hana mamlaka ya kulizungumzia suala hilo.
Mtazamo wa mvutano wa kisiasa nchini Venezuela sasa unatuwama katika hali iwapo Maduro ataruhusu msaada huo kuingia nchini humo, hatua ambayo inatarajiwa katika siku zijazo.
Maduro anakataa kwamba kuna mzozo wa kiutu nchini humo na kusema Venezuela sio nchi ya omba omba. Jeshi la Venezuela limeweka vizuwizi katika daraja linalounganisha nchi hizo mbili kwa makontena katika juhudi za kujaribu kuzuwia misaada hiyo kuingia nchini humo.
kiongozi wa upinzani Juan Guaido , ambaye anaimba jumuiya ya kimataifa kutoa msaada, amesema ni muhimu katika nchi hiyo inayokabiliwa na upungufu wa chakula na madawa.
Urusi na China zamuunga mkono Maduro
Guaido , ambaye anaungwa mkono na mataifa 40, ikiwa ni pamoja na Marekani, anataka kumuondoa madarakani Maduro kufuatia uchaguzi wa mwaka 2018 ambao mataifa mengi yameshutumu kuwa ulikuwa wa udanganyifu. Washirika wa muda mrefu Urusi na China pamoja na mataifa mengine kadhaa yanaendelea kumuunga mkono Maduro.
Kiasi ya wanaharakati wapatao 12 wa haki za binadamu walisimama katika lango la kuingilia katika daraja la kimataifa la Tienditas katika upande wa Colombia, wakidai Maduro aruhusu msaada huo wa dharura kuingia nchini Venezuela. Walipunga bendera wakati magari ya polisi wa Colombia yaliyowabeba polisi waliokuwa na silaha na maafisa wengine yakipita siku nzima. Luis Escobar, raia wa Venezuela ambaye anaishi nchini Colombia baada ya kukimbia taifa lake lililokumbwa na matatizo, amesema mke wake ana kansa ya ziwa ambayo imefika katika hatua ya juu na kumtaka Maduro kukubali msaada.
Akitokwa na machozi , alielezea vipi mkewe alishindwa kupata matibabu nchini Venezuela na kwamba katika wakati walipopata kumuona daktari nchini Colombia, ugonjwa wake ilikuwa tayari umetapakaa mno.
"Niko hapa kwasababu , kwa bahati mbaya, mke wangu anakufa, " Escobar alisema.
"Lakini leo niko hapa kwa ajili ya Wavenezuela ambao wanataabika kama mke wangu. Dunia inapaswa kufahamu juu ya hili."
Kanali wa zamani aungama
Wakati huo huo , waziri wa mawasiliano wa Venezuela , Jorge Rodriguez , alijitokeza katika televisheni akidai kwamba idara ya ujasusi ya Colombia , CIA na mbunge wa upinzani wa Venezuela ambaye anaishi uhamishoni Julio Borges wanahusika na mpango wa kumpindua Maduro.
"Muuaji kama Borges ni lazima aweke kando unafiki," Rodriguez alisema. "hakuna demokrasia , hakuna msaada wa kiutu. Kitu gani atasema, hivi sasa ambapo washirika wake wamemuumbua?
Rodroguez alionesha video ya kile alichosema kuwa ni kuungama kwa kanali mstaafu kutoka katika kikosi cha jeshi la ulinzi la taifa Oswald Garcia Palomo kuwa ni ushahidi wa madai hayo ya njama ya mapinduzi. Mkosoaji mkubwa wa Maduro, Palomo amezungumzia wazi kuhusu kukusanya wanajeshi nje ya nchi kumuondoa kiongozi wa Venezuela kutoka madarakani. Alikamatwa mwezi uliopita baada ya kuingia nchini Venezuela kwa siri akitokea Colombia.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri : Yusuf, Saumu