Miripuko ya mabomu yatikisa Kanisa Ufilipino
27 Januari 2019Mabomu mawili yameripuka nje ya Kanisa wakati wa Misa ya Jumapili kusini mwa Ufilipino, na kuuawa watu 20 na kuwajeruhi wengine 77, maafisa wamesema. Bomu la kwanza liliripuka nje ya Kanisa Katoliki la Kirumi kwenye kisiwa cha Jolo katika mkoa wa Sulu, na la pili liliripuka dakika moja baadae karibu na lango kuu la kuingilia kanisani hapo.
Picha kutoka eneo la tukio zilionyesha mlango, mabenchi ya kanisani na madirisha ya vioo vya Kanisa la Mount Camel vikiwa vimevunjwa vunjwa, na miili ikiwa imetapakaa chini, alisema mpiga picha wa shirika la habari la Ufaransa AFP.
Msemaji wa Rais Rodrigo Duterte amelaani tukio hilo alilolitaja kuwa "kitendo cha ugaidi na mauaji." "Lengo kwa uhakika ni .... ugaidi. Hawa ni watu wasiopenda amani," msemaji wa jeshi kwenye mkoa huo Luteni Kanali Gerry Besana aliliambia shirika la habari la AFP.
Alisema wachunguzi walikuwa wanajaribu kubaini aina ya vilipuzi vilivyotumiwa katika shambulio hilo ili kusaidia kuwabaini washukiwa. Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo ambalo limegharimu maisha ya wanajeshi na pia raia.
Makubaliano ya utawala wa ndani kwa Waislamu
Miripuko hiyo pacha imetokea karibu wiki moja baada ya Waislamu wachache katika taifa hilo lenye Wakatoliki wengi, kupiga kura kuunga mkono utawala wa ndani katika mkoa wao kusini mwa Ufilipino.
Kuundwa kwa mkoa wa Bangsamoro wenye utawala wake wa mdani kwa Waislamu wa Mindanao, ilikuwa sehemu ya makubaliano ya amani ya 2014 kati ya serikali ya Ufilipino na kundi la wapiganaji wa chini kwa chini la Moro Islamic Liberation Front (MILF), ambalo ndiyo kundi kubwa zaidi la waasi.
Ingawa maeneo mengi zaidi ya Waislamu yaliidhinisha makubaliano hayo ya kuwa na utawala wa ndani, wapigakura katika mkoa wa Sulu, iliko Jolo waliyakataa. Kisiwa cha Jolo kimekuwa ngome ya Abu Sayyaf, kundi la Kiislamu lenye itikadi kali lililoorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani na Ufilipino.
Kundi hilo linafahamika kwa kufanya mashambulizi ya mabomu, maauwaji na utekaji nyara. Waziri wa ulinzi Delfin Lorenzana ameamuru usalama uimarishwe mkoani kote, wakati kukiwa na wasiwasi wa kutokea mashambulio zaidi.
"Nimeviagiza vikosi vyetu kuzidisha hali ya tahadhari, kuweka ulinzi kwenye maeneo yote ya ibada na ya umma mara moja, na kuanzisha hatua madhubuti za kiusalama ili kuzuwia mipango ya uadui."
Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW
Mhariri: Oummilkheir Hamidou