Mipaka ya uhuru wa maoni inamalizikia wapi ?
13 Desemba 2017Uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trumpo wa kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, umezusha ghadhabu miongoni mwa waislam ulimwenguni. Maandamano yameripotiwa katika kila pembe ya dunia. Katika maandamano yaliyoitishwa mwishoni mwa wiki mjini Berlin, bendera za Israel zenye nyota ya David zilichomwa moto. Kitendo hicho kimekosolewa vikali na kuzusha mjadala humu nchini, uhuru wa mtu kutoa maoni yake unaishia wapi? Gazeti la "Volksstimme linaandika: "Nuksi ya uamuzi kutoka Marekani imeshaingia Ulaya. Ghadhabu za wapalastina na waislam wanaoishi nchini Ujerumani na barani Ulaya kwa jumla zimechukua sura ya chuki dhidi ya wayahudi, tangu nchini Sweeden, Austria mpaka nchini Ujerumani. Chanzo cha mbali, madhara ya karibu: Ugonvi uliohamishiwa kutoka ardhi tukufu umeripuliwa katika barabara za mjini Berlin. Na hapo viongozi wa kisiasa nchini Ujerumani, ghadhabu zao si za bure. Raia wa Ujerumani wenye asili ya kiyahudi hawastahiki peke yao kumeza machungu ya kinachotokea Israel kwa msaada wa Marekani."
Duru ya kwanza ya kutahmini uwezekano wa kuundwa serikali mpya ya muungano kati ya CDU/CSU na SPD yaanza leo
Miezi miwili na nusu baada ya uchaguzi mkuu na baada ya kushindwa mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano wa Jamaica kati ya wahafidhina wa vyama vya CDU/CSU, waliberali wa FDP na walinzi wa mazingira die Grüne, wawakilishi wa vyama vya CDU/CSU na SPD wanakutana leo usiku kutathmini uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikuu, mashuhuri kwa jina GROKO. SPD wanaingia shingo upande mazungumzoni baada ya kutangaza hapo awali nia yao ya kukalia viti vya upinzani. Wanazungumzia uwezekano wa kuibuka serikali ya ushirikiano, KOKO. Gazeti la Landeszeitung linaandika: "Naiwe serikali ya muungano wa Jamaica, Groko aau KoKo.Yote sawa tu. Kimoja lakini ni dhahiri kinyang'anyiro cha kuania madaraka kimefikia mahala ambapo wananchi wemechoka nacho. Na kinaudhi. Huu si wakati wa kinyang'anyiro kisichokua na maana cha kuania madaraka. Matatizo ya dunia ni makubwa mno ukizingatia suala la mabadiliko ya tabia nchi, Mashariki ya kati, Korea ya Kaskazini, Brexit na mustakbal wa Umoja wa ulaya na yote hayo yanahitaji kushughulikiwa badala ya kupoteza wakati kwa mambo madogo madogo.
Trump alenga sayari ya Mars
Rais wa Marekani Donald Trump anazungumzia mpango wake wa kuigeuza sayari ya mwezi kuwa kituo cha muda kuelekea katika sayari ya Mars. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linajiuliza eti mpango huo unaweza kutekelezwa? "Kutokana na gharama kubwa kupita kiasi na hatari iliyoko, mtu anaweza kujiuliza kama kuna haja kweli ya kuwapeleka watu katika sayari ya Mars. Hakuna chochote ambacho mtambo au robota inayoweza kubuniwa siku za mbele haitoweza kukifanya tena vizuri zaidi hata kumshinda binaadam katika mazingira ya mauti yasiyoepukika katika sayari hiyo na kurejea salama katika sayari ya dunia. Kiu cha kupenda makubwa pekee hakihalalishi kujitosa katika hatari kama hiyo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman