Milio ya risasi yasikika nje ya makazi ya rais Burkina Faso
30 Septemba 2022Milio ya risasi imesikika katika maeneo ya kuzunguuka makaazi ya rais na makao makuu ya jeshi nchini BurkinaFaso leo alfajiri. Serikali imesema tukio hilo linahusishwa na mgogoro wa ndani katika jeshi hilo.
Mwandishi wa habari wa shirika la AFP amesimulia kuona wanajeshi chungunzima wakiwa wamefunga barabara nyingi,kuu za mji mkuu Ougadogou. Serikali ya BurkinaFaso imetoa maelezo kwamba tukio hilo linahusishwa na mgogoro wa ndani jeshini,jeshi ambalo lenyewe lilifanya mapinduzi na kutwaa madaraka kwa nguvu nchini humo mnamo mwezi Januari.
Msemaji wa serikali Lionel Bilgo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mazungumzi yanaendelea kujaribu kupata maelewano bila ya kuzuka matatizo.Milio ya risasi ilisikika majira ya asubuhi leo Ijumaa katika maeneo yaliko makaazi ya rais na makao makuu ya jeshi.
Mkaazi mmoja aliyeshuhudia akisumulia amesema alisikia mirindimo ya risasi mida ya saa kumi na nusu alfajiri na kushuhudia barabara zikifungwa na magari ya kijeshi katika maeneo yanayozunguuka nyumbani kwake ambako ni karibu na makaazi ya rais.
Kwa mujibu wa msemaji wa serikali Lionel Bilgo mgogoro uliopo umetokana na madai yanayohusishwa na mishahara na kwamba mtawala wa kijeshi Luteni Kanali Paul Sandaogo Damiba anashiriki kwenye mazungumzo ya kutafuta mwafaka na wanaohusika.Chanzo kutoka serikalini awali kilithibitisha kwamba Kanali Damiba yuko mahala salama.
Imeelezwa kwamba televisheni ya taifa ilisitisha matangazo kwa masaa kadhaa na hakuna chochote kilichooneshwa.Lakini pia chanzo kingine kutoka serikalini kilisema mazungumzo yanaendelea na wanajeshi wanazidi kuishinikiza serikali kwa kuendelea kukamata vituo vya kimkakati walivyovishikilia toka asubuhi katika mji mkuu Ougadogou.Wanajeshi walionekana katika barabara kuu - zote na hasa kwenye mtaa wa Ouga 2000 lakini pia nje ya kituo cha televisheni ya taifa,kwa mujibu wa mwandishi habari wa AFP.
Mchambuzi mmoja mwandamizi wa masuala ya Afrika Eric Humprey Smith amezungumzia kwamba kinachotokea ni jaribio la mapinduzi, akisema pamoja na kwamba milio ya risasi inawezekana kuwa ishara ya kutokea uasi lakini suala la kuzimwa kwa matangazo ya kituo cha televisheni ya taifa linaonesha zaidi ya hivyo.
Katika mitaa ya mji mkuu Ougadogou baadhi ya wananchi tayari wameshajitokeza wakionesha kuunga mkono kile wanachoamini ni mapinduzi dhidi ya Kanali Damiba, mwanaharakati mmoja wa masuala ya kisiasa Francois Beogo amesikika akisema tunaandamana kuunga mkono mapinduzi iwe imethibitishwa au hayakuthibitishwa.
Hali hiyo inayojitokeza nchini Burkina Faso imeanza kuzusha wasiwasi. Mjini Brussels, Umoja wa Ulaya umesema una wasiwasi na matukio yanayoonekana sasa huko Ougadougou.Msemaji wa masuala ya mambo ya nje na usalama wa Umoja huo wa Ulaya, Nabila Massrali, amesema bado hali haileweki ingawa wameshuhudia kilichotokea tangu asubuhi.
BurkinaFaso imeandamwa na machafuko kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na mapinduzi yaliyomuweka madarakani kanali Damiba baada ya kumuondowa rais aliyechaguliwa na wananchi Roch Marc Christian Kabore.Mtawala huyo wa kijeshi Damiba aliahidi kurudisha utawala wa kiraia ndani ya kipindi cha miaka miwili na kuyamaliza makundi ya wanamgambo nchini humo.
Mwanzoni mwa mwezi huu alimtimua waziri wake wa ulinzi na kujitwika mwenyewe jukumu hilo.Maelfu ya watu wamekufa na kiasi wengine milioni 2 wameachwa bila makaazi kufuatia mapigano tangu mwaka 2015 wakati uasi uliposambaa na kuingia mpaka kwenye nchi hiyo ya BurkinaFaso ambayo toka wakati huo imegeuka kuwa kitovu cha machafuko katika eneo la Sahel.
Na mashambulizi katika taifa hilo yameongezeka tangu mwanzoni mwa mwaka huu licha ya utawala huo wa kijeshi kuahidi kulipa kipaumbele suala la usalama.