Michuano ya Euro 2022 kwa wanawake: Timu za kutizamwa
Michuano ya soka ya Euro kwa wanawake imeanza rasmi huko England ikitarajiwa kuwa na ushindani mkali kwasababu ya timu zenye wachezaji mahiri. Na hizi ndio zinapewa nafasi kubwa ya kupiga soka safi.
Ujerumani
Kikosi cha Martina Voss-Tecklenburg kimesheheni wachezaji kutoka klabu kubwa za Ulaya. Ujerumani itajumuisha wachezaji kinda na wenye uzoefu, lengo ni kufika hadi nusu fainali. Sara Däbritz, ambaye amejiunga na mabingwa wa Ulaya klabu ya Lyon, atatafuta kushinda kombe la kwanza kubwa la Ujerumani tangu mwaka 2013. Lakini hata hivyo kikosi hicho kitamkosa Dzsenifer Marozsan kutokana na majeraha.
Norway
Baada ya kutolewa katika hatua ya makundi ya mashindano ya Euro mwaka 2017, Norway inatafuta kurejesha rekodi safi katika mashindano ikiwa imeshinda mara mbili na kufika fainali mwaka 2013. Ada Hegerberg, mshindi wa kwanza wa kiatu cha dhahabu- Ballon d’Or kwa wanawake 2018, amerejea viwanjani baada ya kukosekana kwa miaka mitano akipinga ukosefu wa usawa katika shirikisho la soka la Norway FA.
Ufaransa
Baada ya kushindwa katika kombe la dunia la 2019 nyumbani, kikosi cha Corinne Diacre kitataka kujiimarisha. Inaweza kuwa vigumu kutokana na kukosekana kwa wachezaji mahiri kama vile Amandine Henry na Eugenie Le Sommer, ambao wameachwa kwenye kikosi. Beki mwenye uzoefu Wendie Renard, wa mabingwa watetezi wa Champions League Lyon, anaongoza timu yenye uzoefu mwingi wa ushindi katika ngazi ya klabu.
Uholanzi
Mabingwa hao watetezi wa ligi ya mabingwa Ulaya watajaribu kutetea ubingwa wao nchini Uingereza, wakati huu ambapo mwingereza Mark Parsons akishika usukani. Mshambuliaji nyota wa Arsenal, Vivianne Miedma ambaye ndiye mfungaji bora wa mabao katika timu ya taifa ya Uholanzi, anatarajiwa kuiongoza timu hiyo katika hatua za mwisho za michuano hiyo.
England
Wenyeji wa michuano hiyo wanajiona kuwa miongoni mwa washindani wakuu. Kikosi hiki kimeundwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji kutoka ligi kuu ya wanawake inayokua kwa kasi, pamoja na vilabu vikubwa vya Uropa. Beki wa pembeni Lucy Bronze amechezea klabu kadhaa kubwa na za hali ya juu na atakuwa akitafuta kupata taji la kwanza kuu kwa England baada ya kukubali ofa ya kuichezea Barcelona muhula ujao.
Uhispania
Wakiwa na kikosi kilichoundwa na takriban vipaji vyote vya La Liga, wachezaji wa Jorge Vilda watatafuta kupata taji la kwanza kabisa la Uropa katika mashindano ya wanawake. Alexia Putellas wa Barcelona, anayechukuliwa na wengi kama mchezaji bora zaidi duniani, ndiye anayetazamwa.
Sweden
Ikiwa na wachezaji wengi kwenye vilabu vikuu vya Ulaya na historia nzuri, Sweden ni moja ya timu za kutazama kwenye mashindano ya Euro. Washindi wa medali ya fedha kutoka Michezo ya Olimpiki ya Beijing watatarajia kushinda kombe kuu kwa ajili ya nchi yao kwa mara ya kwanza tangu kushinda Euro 1984. Kiwango kizuri cha Fridolina Rolfö kutoka Barcelona kinaweza kuwasaidia katika kufikia lengo lao.