1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atakayecheza kwenye fainali ya Copa America?

29 Juni 2015

Michuano ya Kombe la Mataifa ya Amerika ya Kusini - maarufu kama Copa America imeingia nusu fainali nchini Chile ambapo kuna mechi kadhaa za kusisimua zitakachozwa

https://p.dw.com/p/1Fpbh
Fußball Copa America Brasilien vs. Paraguay
Picha: Reuters/J. Adorno

Chile itakutana na Peru katika nusu fainali itakayochezwa leo ikiwa ni mojawapo ya michuano yenye utani mkali zaidi katika kandanda la Amerika Kusini, unaochochewa na siasa, migogoro ya mipaka na vita vya karne ya 19. Chile iliiangusha Uruguay katika robo fainali wakati Peru ikiipiku Bolivia.

Makocha wa timu zote mbili wameelezea matumaini yao ya kupata ushindi ndani ya uwanja. Kando na kibarua cha kucheza dhidi ya Peru, Chile ni lazima iridhike na adhabu iliyotolewa kwa beki wake Gonzalo Jara ambaye atakosa michuano yote iliyosalia ya Copa America baada ya kufungiwa mechi tatu kwa kufanya kitendo cha kashfa dhidi ya mchezaji wa upinzani, Edinson Cavani na kujifanya kuwa ameumia wakati wa mchuano huo.

Chile Fußball Peru gegen Bolivien
Peru iliwabandua nje Bolivia katika hatua ya robo fainaliPicha: Reuters/C. Garcia Rawlins

Shirikisho la Kandanda la Amerika ya Kusini – CONMEBOL pia limelitoza shirikisho la kandanda la Chile faini ya dola 7,500. Kocha Sampaoli lazima aweke mkakati wa kulijaza pengo hilo. Kocha wa Peru Ricardo Gareca aliusifu uwezo wa Chile lakini akasema kikosi chake kiko ngangari kwa kibarua cha leo

Katika nusu fainali ya pili, timu yenye vigogo Argentina, ambayo imecheza vyema lakini bado haijaridhisha katika ufungaji magoli, na Paraguay ambayo imeonyesha mchezo imara, na ambayo haikupigiwa upatu na yeyote kushinda, zinatarajiwa kukutana tena. Lakini mara hii, tuzo ya mpambano huo ni fainali ya Copa America.

Paraguay iliwashangaza wengi kwa kuibandua nje Brazil. Argentina waliwaondoa Colombia Ijumaa iliyopita katika robo fainali kupitia mikwaju ya penalty baada ya mchuano kukamilika kwa sare ya bila bila.

Hata hivyo inashangaza, kwamba huku wakiwa na safu ya mashambulizi inayoongozwa na Lionel Messi, Sergio Aguero, Angel Di Maria na Javier Pastore, halafu wachezaji kama vile Carlos Tevez na Gonzalo Higuain wakiwa kwenye benchi la akiba, bado wanatatizika kutikiza nyavu….licha ya kuwa na nafasi chungu nzima. Acha tuone mambo yatakavyokuwa katika mpambano wa kesho. Mshindi wa mchuano huo atacheza dhidi ya wenyeji Chile au Peru katika fainali ya Jumamosi.

Naam mshindi wa kombe la Copa America wikendi hii hajulikani kwa sasa, lakini bila shaka ukweli wa mambo ni kuwa kocha atakayeongoza timu itakayotwaa kombe hilo, atakuwa Muargentina.

Maana timu zote nne zinaongozwa na makocha wa Kiargentina. Chile inafunzwa na Jorge Sampaoli, Peru ina Ricardo Gareca, Argentina ina Gerardo Martino na Paraguay inaongozwa na Ramon Diaz. Kila la kheri kwa Waargentina hao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Rueters
Mhariri:Iddi Ssessanga