Michel Platini ahojiwa na mwendesha mashitaka Uswisi .
31 Agosti 2020Mwanasoka nyota wa zamani wa Ufaransa Michel Platini amewasili katika ofisi ya mwendesha mashitaka wa Uswisi leo asubuhi akitakiwa kwa mahojiano juu ya malipo ya dola milioni 2 aliyopokea kutoka FIFA mwaka 2011.
Platini rasmi ni mshukiwa kwasababu ya malipo hayo ambayo yamepelekea kuondolewa kwake madarakani kama rais wa shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA, na kama mgombea wa kiti cha urais wa FIFA, ambako wachunguzi wa serikali kuu ya Uswisi walifichua madai hayo miaka mitano iliyopita.
Platini nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa mwenye umri wa miaka 65 anashukiwa kuwa mshirika wa uhalifu wa ubadhirifu, wa matumizi mabaya ya fedha na kitendo cha kughushi, kwa mujibu wa nyaraka zilizoonekana na shirika la habari la Associated Press mwezi Juni. Platini ambaye alikuwa makamu wa shirikisho la kandanda duniani FIFA, hakutoa maelezo kuhusu kesi hiyo leo wakati akiingia katika makao makuu ya ofisi ya mwendesha mashitaka.